VIONGOZI wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) na Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), wamewataka wanachuo waliojiunga na vyuo hivyo, kujifunza matumizi ya kompyuta ili kwenda sambamba na mahitaji ya karne ya sasa ya sayansi na teknolojia.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wakati wa uzinduzi wa mwaka wa maasomo wa 2010/2011, viongozi hao walisema ni lazima kwa wanafunzi wa vyuo vikuu, kuwa na maarifa ya matumizi ya kompyuta kwa kuwa masuala mengi yanayohusu masomo yanayopatikana kwa njia ya mtandao.
Mkurugenzi wa OUT katika Kituo cha Morogoro, Dk Said Massomo, alisema si jambo la kushangaza kwa sasa kuwaona baadhi ya wanafunzi wa vyuo vikuu wakiwa bado hawajui kutumia kompyuta wakati wanafunzi wa shule za msingi, wakizitumia kwa usahihi zaidi.
"Msiogope kujifunza, tumieni muda mnaoupata kwenda kwenye Internet café zilizoko hapa mjini utaweza kupata mambo mengi sana yanayohusiana na masomo umnayochukua," alisema.
Alisisitiza kuwa tofauti na ilivyo kwa wanafunzi wa vyuo vingine, wanafunzi wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, lazima wajijengee nidhamu ya kutafuta mambo wenyewe, kujipangia ratiba na kuifuata na kuheshimu muda.
Akizungumza na wanafunzi wa chuo hicho mkoani Morogoro juzi,Dk Massomo alisema si mambo yote ambayo wanafunzi wanaweza kuyapata kupitia katika vitabu na machapisho, lakini kwa kiasi kikubwa yanaweza kupatikana katika mtandao wa kompyuta.
Kwa upande mwingine, Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu cha Sokoine, Balozi Nicholus Kuhanga, akizungumza katika uzinduzi wa mwaka wa masomo, alisema SUA imeanzisha mafunzo ya kompyuta, ili kila mwanafunzi wa chuo hicho aweze kuwa na msingi wa matumizi ya kompyuta.
Alisema ingawa chuo hakina kompyuta za kutosha, lakini ni wajibu wa wanachuo kuhakikisha kuwa wanatumia njia nyingine kupata kompyuta kupata mambo mbalimbali ya msingi katika masomo yao.
Balozi Kuhanga aliwaonya wanafunzi waliojiunga na chuo hicho kutokukubali kupata shahada bandia kwa kutumia njia za hujuma mbalimbali ikiwa ni pamoja na kukodisha watu wa kuwafanyia mitihani yao.
"Heri kutoendelea na masomo kuliko kupata shahada bandia, lazima kila Mtanzania awe mzalendo kwa kufanya vitu vya haki, nchi hii itasonga mbele kwa watu kuweka mbele uzalendo," alisema mwenyekiti huyo wa baraza la chuo.
Alisema katika dunia ya sasa, kuna watu wengi ambao wanatembea na vyeti bandia vya ngazi mbalimbali wanavyovipata kutoka katika vyuo bandia au vyeti vya ndugu zao na kuvitumia katika kutafutia kazi.
Chanzo:Mwananchi
Loading...
Post a Comment
CodeNirvana