Ndugu Zangu,
JANA usiku katika pekuapekua zangu za idhaa za redioni, nikakutana, kwa mara ya kwanza, na Redio Imaan FM. Inatangaza kutoka Morogoro. Nilichosikiliza kilikuwa kipindi maalum cha marudio kutoka Jumapili iliyopita. Niseme neon moja tu na kwa msisitizo: NILISHTUKA.
Hakika, kilichokuwa kikirushwa hewani ni matangazo ya uchochezi. Kuchochea uhasama baina ya Watanzania Waislam na Watanzania wenzao Wakristo. Nilijiuliza, kama taifa tunakwenda wapi? Na maswali yakawa mengi. Je, Tume ya Utangazaji inafahamu kinachoendelea au imelala usingizi? Je, watu wetu wa Intelijensia hawana taarifa za Kiintelijensia juu ya kinachooendelea?
Naam. uzoefu unatufundisha, kuwa kuwasha moto ni jambo jepesi sana, lakini, kuuzima moto, yaweza kuwa ni kazi ngumu sana.
Moto ulioanza kwenye nyumba moja ya nyasi kijijini, waweza kusambaa haraka na hata kuteketeza nyumba nyingine, mali na kuhatarisha maisha.
Nimekumbushia mara kadhaa, kuwa historia ni mwalimu mzuri. Mwezi Aprili 6, mwaka 1999 katika iliyokuwa Hoteli ya Kilimanjaro, Bi Joy Mukanyange , aliyekuwa Balozi wa Rwanda hapa Tanzania, alituambia Watanzania juu ya kile alichokiona lakini sisi Watanzania hatukukiona. Ilikuwa ni katika mjadala rasmi wa kumbukumbu ya mauji ya kimbari ya watu wa Rwanda ya mwaka 1994.
Bi Mukanyange alisema: ” Naogopa., kwani nimeanza kuona dalili zinazojengeka za mgawanyiko wa kidini nchini Tanzania na eneo lote la Maziwa Makuu, hali ambayo inaweza kusababisha mauaji ya halaiki kama yale yaliyotokea nchini mwetu mwaka 1994,” alisema Balozi huyo wa Rwanda kabla ya kuendelea kutoa ufafanuzi wa historia ya Rwanda na matukio yaliyosababisha maujai yale ya Wanyarwanda ya wao kwa wao. Ni kauli ya kuitafakari kwa makini.
Mimi sasa naamini, kuwa Afrika mvunja nchi si mwananchi, bali ni mwanasiasa. Ni kwa kutanguliza mbele maslahi ya kisiasa badala ya kitaifa. Masikini nchi yetu, Watanzania hawana udini ila kuna wachache, na hasa wanasiasa, walio tayari kutumia mtaji wa udini kutimiza malengo yao. Inasikitisha sana, kuwa baadhi ya wanasiasa, hata kwa kutumia udini, wameamua kutupitisha Watanzania katika njia isiyo salama. Ili mradi, malengo yao yatimie.
Watanzania tukubali sasa, kuwa nchi yetu imepatwa na bahati mbaya ya baadhi ya Watanzania wenzetu kuanza kupandikiza mbegu za chuki miongoni mwetu. Kuna wanaotaka tuanze kubaguana kwa misingi ya kidini. Hili ni jambo la hatari sana.
Taratibu tumeanza kuizoea misamiati ya sisi na wao. Mathalan, sisi Wakristo na wao Waislamu. Sisi Wachagga na wao Wazaramo. Tunasahau, kuwa katika nchi yetu hii hakuna Sisi na Wao, kuna SISI tu.Tutakapokumbwa na maafa ya kitaifa watakaoathirika ni SISI, hakutakuwa na WAO.
Hatari kubwa ninayoiona ni tatizo la baadhi ya Watanzania kuwa na ufahamu mdogo juu ya dunia tunayoishi sasa, kibaya zaidi,ufahamu mdogo wa historia yetu. Uelewa wa historia ya jamii husika ni jambo muhimu sana.
Kiumbe huwezi kuelewa ya leo, kesho na kesho kutwa kama huelewi ya jana. Kuielewa historia yako ni kuelewa ulipo na unakokwenda.
Dalili tunazoziona sasa za kupandikiza mbegu za chuki kwa misingi ya udini si dalili njema. Haya yatatupelekea kwenye maafa.
Hii ni nchi yetu. Katika ulimwengu tunamoishi kuna mamilioni ya watu wasio na nchi. Wahenga wetu walishiriki katika kuijenga nchi hii, wametutarajia sisi tuendelee kuijenga na kuilinda hadhi ya nchi hii.
Muda wetu wa kuishi humu duniani ni mfupi sana. Tuyachambue matatizo halisi ya jamii yetu. Kisha tusiishie kwenye kuyaorodhesha, hiyo ni kazi rahisi sana. Tutafute njia ya kuyatatua matatizo hayo.
Hatuna haja ya kubaguana kwa misingi ya ukabila, dini na rangi. Sisi wote ni Watanzania. Tuna historia ya kujivunia. Ni historia yetu wenyewe.
Mtanzania halisi na mkweli kwa nchi yake atazungumzia matatizo ya Tanzania kwa ujumla wake. Hatakuwa na sababu ya kunyoosha kidole kwa Wahindi, Walutheli, Waprotestanti, Wasabato, Wakatoliki, Washia, Wasunni, Waismailia, wenye kuamini jadi, Wazaramo, Wagogo au Wachagga, kwamba ndio wa kulaumiwa.
Wenye kuathirika na umasikini wa nchi hii ni wengi mno. Si Wakristo peke yao, si Waislamu peke yao, si Wapagani peke yao, si Wamachinga peke yao na si Wazaramo peke yao.
Wahenga walisema ”kamba hukatikia pabovu”. Kamwe huwezi kuwavuruga Watanzania na kuwafanya wachinjane kwa sababu za kudai kuna upendeleo wa ukabila au wa kisiasa. Nchi hii ina makabila zaidi ya 125 na utitiri wa vyama vya siasa.
Mahala ambapo unaweza kuwagawa Watanzania na hata kufanikiwa wachinjane ni kwenye masuala ya imani. Tusikubali dini iwe ndiyo penye ubovu kwenye kamba inayotuunganisha Watanzania. Mungu Ibariki Tanzania.
Maggid
Dar es Salaam
Januari 19, 2011
www.mjengwa.blogspot.com
Loading...
Post a Comment
CodeNirvana