Featured

    Featured Posts

    Social Icons

    .
Loading...

Sitta na Posho !

WAZIRI wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta amejitosa kwenye mjadala wa posho ulioanza bungeni hivi karibuni akieleza kuwa suala la kujadili posho za wanasiasa na watendaji wengine linatakiwa kuanzia ngazi ya chini.

Alisema juzi katika mdahalo ulioandaliwa na Jumuia ya Wanafunzi wa Chuo Kikuu Mzumbe kuwa fedha nyingi zimekuwa zikipotea na hata wananchi wanapojaribu kuhoji hakuna maelezo yanayotolewa kwao na baadhi ya watendaji wa serikali zikiwamo za vijiji.

Sitta, ambaye ni Mbunge wa Urambo Mashariki (CCM) alisema kuwa malumbano yanayoendelea bungeni kuhusu posho za wabunge na watumishi wengine wa serikali hayana msingi na badala yake wanataaluma ndio wangetakiwa kulipwa vizuri tena kwa fedha nzuri kuliko wanasiasa.

Alisema kuwa wanataaluma wangepaswa kulipwa zaidi kuliko wanasiasa kutokana na kuwa wamehangaikia taaluma zao kwa miaka mingi kuliko wanasiasa, akieleza kuwa siasa ni kitu cha kujitolea.

"Sioni sababu ya wabunge kuendelea kujadiliana na kubishana juu ya suala hili la posho.

“Kinachotakiwa ni kumlipa vizuri mtu aliyehangaikia taaluma yake tena kwa muda mrefu, inafaa apewe mshahara mzuri kulingana na taaluma yake, lakini kwa nchi yetu wataalamu wanalipwa mishahara midogo ambayo haikidhi hata mahitaji yao ya msingi.

"Matokeo yake, wengi wakishamaliza elimu yao wanakimbilia nje ya nchi kufanya kazi au kugeukia siasa,” alisema Sitta na kuongeza:

Sitta ambaye alikuwa Spika wa Bunge la Tisa la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliuambia mdahalo huo wa kujadili masuala ya Jumuia ya Afrika Mashariki ulioandaliwa na Jumuia ya Wanafunzi wa Chuo Kikuu Mzumbe kuwa hali hiyo haina budi kubadilishwa.

“Inashangaza kuona fedha nyingi zinapotea kuanzia vijijini na watendaji wake wamekuwa wakijilipa na kufanyia mambo yao bila kushirikisha wananchi na hata kutowasomea mapato na matumizi ya kijiji husika bila ufuatiliaji na wala hakuna jambo lolote linaloweza kufanyika,”alisema.

Pia, aliwataka wananchi hususani vijana kuwa wawajibikaji zaidi na kuweka uzito katika mambo ya msingi ya taifa na kuhakikisha wanakemea wala rushwa na wale wanaojitajirisha kwa maslahi yao na kuwanyonya watu wa hali ya chini.

Alisema ndani ya Serikali ya Tanzania kuna tatizo la uwajibikaji na watumishi wengi wamekuwa wakifanya kazi kwa mazoea na kujisahau kuwa wanatakiwa kuwahudumia wananchi katika masuala ya kimaendeleo.

Kwa upande wao, wanafunzi walishiriki mdahalo huo walihoji ni jinsi gani wananchi wa Tanzania walivyoandaliwa katika kuleta ushindani katika Jumuia ya Afrika Mashariki kwani kila mara wameonekana kuwa nyuma katika ajira kwenye jumuia hiyo.

“Katika hili, wanasiasa wameonekana kuwa ndio wanaoharibu mfumo mzima kutokana na kuweka siasa zaidi mbele badala ya kutenda kazi ya kushirikisha wananchi hasa wa hali ya chini,”alisema Christian Makala, mwanafunzi wa mwaka wa pili wa Kitivo cha Sheria.

Alisema wanasiasa wengi wanapokuwa majukwaani hasa wakati wa kuomba kura wanaonekana wazalendo, lakini pindi wanapopata madaraka ikiwamo kuingia bungeni hubadilika na kujisahau na kukubaliana na mambo kwa maslahi ya vyama vyao.

Chanzo:Mwananchi
author

This post was written by: Author Name

Your description comes here!

Get Free Email Updates to your Inbox!
© Copyright Udaku Kijiweni
Back To Top