SPIKA wa Bunge, Anne Makinda amemvutia pumzi Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe kwa kumuongezea muda wa kuthibitisha madai yake kuwa Baraza la Mawaziri lilishawishiwa na watu kulifuta Shirika Hodhi la Mali za Mashirika ya Umma (CHC) kwa faida ya wachache.
Akisoma taarifa kwa wabunge baada ya kipindi cha maswali na majibu jana, Spika Makinda alisema jitihada za Zitto kuwasilisha ushahidi huo ziligonga mwamba kwa kuwa ofisi ya Spika imekataa kumsaidia kumpatia nyaraka za vikao vya Baraza la Mawaziri.
"Waheshimiwa wabunge itakumbukwa kuwa tarehe 23 mwezi huu, Mheshimiwa Zitto wakati akichangia Azimio la Serikali kutaka kuliongezea uhai Shirika Hodhi la Mashirika ya Umma (CHC), alitoa tuhuma bungeni kwamba Baraza la Mawaziri, limerubuniwa kufikia maamuzi hayo," alisema Makinda na kuongeza:
"Itakumbwa pia kuwa baada ya kauli hiyo, nilimtaka (Zitto) alete ushahidi ifikapo tarehe 29 Juni yaani leo. Sasa kwa kuwa siku yenyewe ya kuleta ushahidi ni leo, naona bora nitoe taarifa rasmi kuhusu nini kilichotokea katika kipindi chote hiki".
Makinda alisema kuwa Zitto alimwandikia barua kuomba Bunge kumsaidia kupata nyaraka hizo ili aweze kuthibitisha madai yake akitumia kifungu cha 10 cha Sheria ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge, Sura ya 296
"Kwamba siku ile ile ya tarehe 23, Mheshimiwa Zitto aliniandikia barua kuniomba nimsaidie kumpatia nyaraka za Kikao cha Baraza la Mawaziri kilichopitisha uamuzi huo. Amefanya hivyo kwa kutumia Kanuni ya Haki, Sura na Madaraka ya Bunge zinazompa haki mbunge kuiomba ofisi ya umma kumpa nyaraka anazozihitaji,"alisema.
Makinda alisema kwa kuwa nyaraka alizoamba Zitto ni za siri na haziwezi kutolewa, hivyo ofisi yake haiwezi kumsaidia kuzipata.
"Waheshimiwa wabunge taratibu za Baraza la Mawaziri kwa uelewa wangu nyaraka alizoziomba Zitto ni za siri na haziwezi kutolewa, Bunge pia limewahi kuarifiwa hivyo na Spika wa Bunge la Tisa tarehe Mosi Julai 2008, wakati akitoa uamuzi kuhusu suala la Nazir Karamagi kwa madai yake kuwa uamuzi wa kuongezwa muda wa mkataba wa TICTS, ulifanywa na Baraza la Mawaziri. Hivyo ofisi yangu haiwezi kumsaidia Kabwe Zitto nyaraka alizoamba,"alisema Makinda.
Alisema katika maelezo yake bungeni, Juni 23, Zitto alizungumza kwa kurudia na kusisitiza kuwa ana uhakika wa kuthibitisha anachokisema, hivyo uamuzi wa kumtaka mbunge huyo kuthibitisha upo palepale isipokuwa atafanya hivyo Jumatatu, Julai nne.
Juni 23 mwaka huu, Zitto alichafua hali ya hewa bungeni na kuzua mvutano mkubwa kati yake na mawaziri baada ya kueleza kuwa Baraza la Mawaziri limeshawishiwa na watu kulifuta CHC kwa faida ya wachache.
Chanzo:Mwananchi.
Loading...
Post a Comment
CodeNirvana