Featured

    Featured Posts

    Social Icons

    .
Loading...

CCM Arusha kutumia viongozi wa mila kuidhibiti Chadema

Monday, 21 May 2012
Peter Saramba, Arusha
BAADA ya wimbi la viongozi na wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wilayani Ngorongoro wanaohamia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kuendelea kushika kasi, chama hicho tawala sasa kimeamua kutumia viongozi wa kimila (Malaigwanan) kukabiliana nalo.

Habari zilizopatikana kutoka Ngorongoro na kuthibitishwa na viongozi
wa vyama vyote viwili wilayani humo, zinaeleza kuwa kikao cha kwanza
cha viongozi wa mila kinatarajiwa kufanyika leo katika Kijiji cha Endulen ambako juzi wana CCM 415 pamoja na mwenyekiti wa kijiji walihamia Chadema.

Akizungumza kwa njia ya simu jana, Mwenyekiti wa CCM na Diwani wa Kata ya Endulen, James Moringe alisema yeye ndiye aliyeitisha kikao hicho cha wazee kwa nia ya kujadili mambo kadhaa kuhusu musthakabali ya kata hiyo kijamii, kisiasa na kiuchumi.

“Pamoja na kuzungumzia mustakhabali ya maendeleo ya kata yetu, lakini pia tutazungumzia taarifa za baadhi ya viongozi na wana CCM kudaiwa kuhamia upinzani, utakuwa ni mkutano mkubwa utakaoshirikisha wazee wa kimila kutoka sehemu mbalimbali wilayani Ngorongoro,” alisema Diwani Moringe.

Alisema CCM wamelazimika kuchukua hatua ya kuitisha kikao cha wazee siyo kwa nia ya kuwazuia wanaotaka kuhamia upinzani kufanya hivyo, kwani ni haki yao kikatiba, bali kujitathmini na kujipanga upya
kuepuka kuendelea kukimbiwa na viongozi na wanachama wengi.

Wakati Mwenyekiti huyo wa CCM akidai kikao hicho kinalenga kujitathmini na kujipanga, wenzake wa Chadema wanadai kinalenga kuwatisha waliohamia upinzani kurejea chama tawala kuepuka laani ya
wazee.

Akizungumza kwa njia ya simu jana, Katibu wa Chadema Kata ya Endulen, Denis Ole Supa ‘Babuu’ alisema, lengo la kikao hicho cha Malaigwanani ni kuwabembeleza waliohamia upinzani kurejea CCM na watakaokataa wametishiwa kulaaniwa.

“Ili kukabiliana na hila hizo, nasi Chadema tumewaita Malaigwanani
wetu ambao miongoni mwao walialikwa kwenye kikao cha CCM kwa ajili ya kuweka mikakati ya kujibu mapigo kwa kufanya maombi maalum kukabiliana na laana itakayotolewa,” alisema Ole Supa

Alisema wazee wengi wa mila wameeleza kushangazwa na kitendo cha viongozi wa CCM kutaka kuwaingiza kwenye masuala ya kisiasa, ambayo siyo moja ya majukumu yao kimila na kuahidi kuwapa Chadema taarifa na mbinu zote zitakazopangwa dhidi yao.

Mwenyekiti wa Chadema, Wilaya ya Ngorongoro, Revocatus Parapara alisema vitisho vya kutumia laana ya wazee dhidi ya waliohamia Chadema pia vinatolewa kwa wananchi 400 wa Kijiji cha Sinoni waliojiengua kutoka CCM hivi karibuni.

Kwa upande wake, Katibu wa Chadema Mkoa wa Arusha, Mchungaji Amani Golugwa amewataka wote waliojiengua CCM na kujiunga na chama hicho kikuu cha upinzani kuwa imara katika uamuzi wao bila kujali vitisho vya kisiasa wala laana za kimila kwani uanachama wa chama chochote cha siasa ni hiari na haki binafsi ya kila raia.

Matumizi ya viongozi wa mila kwa maslahi ya kisiasa iliwahi kushuhudiwa katika kampeni za uchaguzi mdogo wa Ubunge Jimbo la Arumeru Mashariki ambako Washili wa jamii ya Meru waligawanyika pande mbili, moja likiunga mkono chama tawala na lingine upinzani.

Katika tukio hilo lililoacha kovu katika imani na ushawishi wa Washili Meru ambao waligawana kiukoo katika kuwaunga mkono wagombea huku wale wa Ukoo wa Sumari wakiongoza kampeni za aliyekuwa mgombea wa CCM, Sioi Sumari na wale wa Ukoo wa Nassari wakimuunga mgombea wa Chadema, Jashua Nassari aliyeibuka mshindi.

Na Mwananchi.
author

This post was written by: Author Name

Your description comes here!

Get Free Email Updates to your Inbox!
© Copyright Udaku Kijiweni
Back To Top