Featured

    Featured Posts

    Social Icons

    .
Loading...

HOTUBA YA NAIBU KATIBU MKUU CHADEMA Ndg. ZITTO KABWE KWA WANACHADEMA WANAOISHI MAREKANI – MARYLAND, VIRGINIA NA DC

27.05.2012

Tumekutana leo wakati ambao Taifa letu lipo katika mpito wa mambo mengi sana. Kufuatia shinikizo kubwa kutoka chama chetu cha CHADEMA na asasi nyingine za kiraia ikiwemo viongozi wa dini, tupo katika mchakato wa kuandika upya katiba ya nchi yetu. Lakini pia kuna muamko mkubwa sana wa haki za kiraia na haki za kisiasa katika Taifa letu hivi sasa. Watanzania, kuliko wakati mwingine wowote katika historia ya nchi yetu, wameamka na kutaka mabadiliko ya kisiasa na hasa kutaka kabisa uongozi mpya wa nchi kutoka chama kingine tofauti na chama kinachoongoza hivi sasa. Huu mpito pia, Mpito wa kutoka chama kimoja hodhi kwenda mfumo wa kweli wa vyama vingi vya siasa. Watanzania wameamka sana kujua rasilimali za nchi yao na kutaka kutokomeza rushwa na ufisadi na matumizi mabaya ya utajiri wa nchi. Huu ni mpito wa kutoka viongozi wanaojali maslahi yao binafsi na kwenda kwa viongozi wawajibikaji na wenye uchungu wa kuendeleza nchi yetu na watu wake.

Mpito wowote unapaswa kuongozwa vyema. Unapaswa kushirikisha wananchi wote bila kujali wapo sehemu gani ya Dunia. Chama chetu kipo mstari wa mbele kuongoza mpito tulionao Tanzania. Licha ya kuongoza juhudi za kuwa na Katiba mpya itakayohakikisha HAKI na Wajibu wa Watanzania, lakini pia tumekuwa tukiendelea kupambana na rushwa na ufisadi. Pia tumekuwa tukiendelea kuhakikisha utajiri wa nchi yetu unatumika kwa manufaa ya Watanzania. Hatujatetereka hata kidogo na hatutateterekea kuhakikisha Watanzania wanakuwa na Taifa lenye demokrasia iliyokomaa, lenye maendeleo na ustawi wa watu wake (Developmental Democratic State).

Licha ya kwamba tupo Upinzani, lakini hatua mbalimbali tulizochukua zimeleta mabadiliko makubwa katika nchi yetu. Kuanzia vuguvugu la Buzwagi mpaka kuibuliwa kwa maskandali ya EPA na mpaka kutajwa kwa orodha ya Mafisadi nchini pale MwembeYanga. Hata hivi karibuni juhudi za Bunge kutaka Uwajibikaji Serikalini zilizoongozwa na CHADEMA zimeleta mabadiliko. Inawezekana mabadiliko hayo sio kama tutakavyo, sio kamili, lakini ni hatua ambayo tumepiga. Tutaendelea kama chama cha siasa sio tu kusema na kupiga kelele kuhusu uoza uanaofanyika Serikalini (maana ndio kazi yetu kikanuni) lakini pia kutoa masuluhisho ya matatizo ya nchi yetu na kusukuma kupitia Bunge mabadiliko chanya yanayotakiwa ili kuleta mabadiliko nchini.

Ni matumaini yangu kwamba Watanzania wanaoishi nje ya nchi, kokote walipo watashiriki pamoja nasi katika vuguvugu (movement) hili la kuleta mabadiliko katika Taifa letu. Hampaswi kukaa na kutazama, bali mnapaswa kushiriki kikamilifu maana hii ni nchi yetu sote. Ni wajibu wa kila mmoja wetu kuhakikisha nchi yetu inakuwa na demokrasia na ustawi wa watu wake.

Hali ya Uchumi wa Nchi

Tumekuwa moja ya nchi ambazo uchumi wake unakua kwa kasi zaidi duniani. Katika kipindi cha muongo mmoja uliopita uchumi wa Tanzania umekuwa ukikua kwa wastani wa asilimia 6. Kazi hii ya ukuaji ukilinganisha na kiwango cha ukuaji wa idadi ya watu (ambacho ni 2.8%) ingeweza kupunguza umasikini kwa zaidi ya 50% katika kipindi hicho. Hata hivyo Umasikini Tanzania umebakia ni mkubwa ambapo zaidi ya Watanzania 37 katika kila Watanzania 100 hawana uhakika wa mlo mmoja kwa siku. Idadi ya Watanzania masikini wa kutupwa (wenye kipato cha chini ya tshs 500 kwa siku) imeongezeka kutoka watu milioni 12 mwaka 2007 mpaka watu milioni 15 mwaka 2011. Ukitaka kujua wingi huu ni wa kiwango gani, chukua idadi ya watu wa Nchi ya Botwasana, Namibia, Swaziland na Lesotho haikaribii idadi ya Watanzania wenye mashaka ya mlo mmoja kwa siku. Idadi ya watu wa Denmark, Netherlands, Norway na Uholanzi kwa pamoja ndio sawa na idadi ya Watanzania masikini. Kwa nini?

Ni kitendawili. Ni nadra kukuta uchumi unaokua kwa kasi kama wetu ukizalisha masikini zaidi. It’s a paradox of a fast growing economy and increasing poverty. Kwa miaka kumi ambayo tumeiangalia (2000 – 2010) tumeshuhudia kwa dhahiri kabisa kushindwa kwa sera za kuondoa umasikini zinazotekelezwa na Serikali ya CCM.

Masikini wa Tanzania wapo vijijini zaidi. Uchumi wa vijijini kwa kipindi cha muongo mmoja umekua kwa wastani wa asilimia moja tu. Flat lining. Kwa hiyo uchumi unaokua hivi sasa sio uchumi wa Watanzania bali ni uchumi wa watu wachache kwenye sekta chache kama madini, mawasiliano na ujenzi. Watanzania walio wengi walioko vijijini wanaendelea kuandamwa na ufukara bila juhudi mahususi za kuwasaidia. Tumesema na tunarudia kusema kwamba ni lazima kubadili mwelekeo wa mipango yetu na kujikita kwenye maendeleo vijijini. Kama chama tunaendelea kusema jambo hili ndani ya Bunge na pia kuwaelimisha wananchi kwenye mikutano yetu ya hadhara.

Mfumuko wa Bei umefikia kiwango cha juu sana cha 19% na hivyo hata mikopo katika mabenki imekuwa ghali hadi kufikia riba ya 23% na zaidi. Mfumuko wa bei unaongozwa na bei ya vyakula. Katika hali ya kawaida, kupanda kwa bei za vyakula kungemnufaisha mkulima lakini hali sio hiyo Tanzania. Mkulima bado anauza mazao yake kwa bei za vijijini ambazo ni ndogo na zinaamuliwa na wachuuzi wa mijini. Lakini mkulima huyu anaponunua bidhaa za matumizi yake kama sukari, mafuta ya taa, nguo nk ananunua kwa bei za mijini ambazo zimeathiriwa vikali na mfumuko wa bei. Hivyo mfumuko wa Bei unamuathiri zaidi mwananchi masikini kabisa. Serikali imekuwa mlalamikaji kama wananchi wengine. Mfumuko wa Bei utapungua kwa kuongeza uzalishaji wa chakula, kuimarisha miundombinu ya vijijini na kupunguza gharama za Nishati kama hasa Umeme. CHADEMA inaendelea kuisukuma Serikali kuchukua hatua ili kupunguza makali ya maisha kwa wananchi. Hatua za muda mfupi zihusishe nafuu ya kodi kwenye bidhaa zinazotumiwa na wananchi kwa wingi.

Hata hivyo bado matumizi ya Serikali ni makubwa mno kwenye masuala ambayo hayana uhusiano na kuendeleza watu. Bado bajeti ya posho mbalimbali, safari za nje na hata matumizi makubwa ya magari ya serikali ni kubwa mno kulinganisha na hali yetu ilivyo. Katika matumizi haya pia kuna ufisadi mkubwa sana. CHADEMA inaendelea kuanisha masuala haya na kukemea na kuchukua hatua pale inapobidi.

Uwezo wetu wa kukusanya mapato ni changamoto kubwa. Mapato mengi yanapotea kama misamaha ya kodi ambayo sasa imefikia tshs 1.3trn kwa mwaka. Mapato mengine hayakusanywi kwa sababu ya ukwepaji kodi uliokithiri. Kodi kwenye Sekta ya Madini imekuwa ni mjadala wa muda mrefu sana. Sheria ya madini ya mwaka 1998 na Sheria za Fedha ya mwaka 1997 ziliweka mfumo wa kinyonyaji kabisa ambao ulikuwa unafaidisha makampuni ya uchimbaji madini kuliko Taifa. Sheria mpya ya madini ya mwaka 2010 ambayo ilitokana na kazi kubwa tuliyofanya ndani ya Bunge pamoja na Mashirika yasiyo ya kiserikali imeweka mfumo bora zaidi. Hata hivyo makampuni ya Madini yaliweka mgomo kwenye sheria mpya kwa kukataa kuanzisha miradi mipya na hata kukataa kuhamia kwenye sharia mpya. Sheria mpya inataka Serikali kuwa na hisa kwenye kila mgodi, hisa za kampuni za madini kuorodheshwa katika Soko la hisa la Dar es Salaam na kulipwa kwa mrahaba mpya wa asilimia 4 kwa kanuni mpya ya kukokotoa mrahaba (from Netback Value to Gross value) ambayo ingeongeza mapato ya Serikali maradufu. Kwa miaka Serikali imekuwa inapoteza mapato kwa kutotekelezwa kwa sharia mpya. Nimesikia kuanzia mwezi huu kampuni ya Barrick imeanza kulipa mrahaba mpya. Tutataka maelezo ya Serikali kuhusu kampuni nyingine na pia mrahaba wa miaka ya nyuma. Ni lazima Serikali ihakikishe nchi inafaidika na rasilimali zake.

Tunaenda kwenye Uchumi wa Gesi Asilia. Makampuni mawili makubwa duniani yamegundua Gesi Asilia nchini kwa kiwango kikubwa sana. Hivi sasa Tanzania ina Utajiri wa Gesi ulitothibitishwa wa 20TCF na makadirio yanaonyesha kuwa tutafika 85TCF katika kipindi kifupi sana. Bado kuna meneo yanaendelea kufanyiwa utafutaji kutokanana vitalu vilivyogawiwa. Hata hivyo hatuna Sera na Sheria ya kusimamia vema sekta hii na hasa yenye kuhakikisha Uwazi na Uwajibikaji. Hatuna pia Sheria ya kusimamia mapato yanayotokana na Gesi Asilia (Petroleum Revenue Management Act). Hatutaki kurudia makosa yaliyofanyika kwenye sekta ya Madini. Tunataka Gesi Asilia itumike kwa maendeleo ya watu wetu.

Tumependekeza kwamba Vitalu vipya vya kutafuta mafuta visitolewe kwa sasa (moratorium) mpaka hapo Sera mpya, Sheria mpya na mfumo bora wa matumizi ya Fedha zitakazotokana na Mafuta na Gesi ziwepo. Pia shughuli za utafutaji katika vitalu vya sasa zitaongeza thamani ya vitalu vijavyo na hivyo nchi kufaidika zaidi. Tumependekeza pia kwamba ni lazima kuweka mfumo mzima wa uwazi na uwajibikaji katika sekta ili kujipanga vyema na kuepuka yaliyowakuta wenzetu wenye utajiri kama huu ambao uligeuka balaa. Tatu tumependekeza kusomesha Watanzania kwa ngazi zote. Mafundi mchundo kupitia VETA na Mafundi wa kati kupitia Vyuo vya Ufundi. Muhimu zaidi tunataka kijengwe Chuo Kikuu kikubwa Mtwara chenye Kampasi Lindi ambacho kitakuwa ni kituo cha kufundisha sio watanzania tu bali Waafrika wengine kuhusiana na masuala haya. Ujenzi wa Chuo Kikuu Mtwara unapaswa kuanza mara moja bila kuchelewa.

Kutokana na uzoefu tuliupata katika sekta ya Madini na kupitisha sharia mbaya Bungeni, tunaona kwamba suala la Gesi tukabe kila mahala ili kuhakikisha nchi inafaidika. Historia inatuonyesha kwamba Nchi nyingi za Kiafrika zenye utajiri wa Gesi na Mafuta hazina demokrasia, zimegubikwa na uvundo wa ufisadi na watu wake ni masikini. Tunataka kuonyesha Dunia kwamba inawezekana kuwa nan chi ya Kiafrika yenye utajiri mkubwa wa Mafuta na Gesi na ikawa ya kidemokrasia, isiyo na ufisadi na yenye watu wenye ustawi. Sio kazi rahisi lakini tumedhamiria. CHADEMA haitakaa tu kuona utajiri wan chi unatapanywa hovyo. Tumesema na kusimamia kwenye Madini, tunatoa mwongozo kwenye Mafuta na Gesi.

Katiba

Ninajua Watanzania mnaoishi nje mna shauku kubwa ya kujua ushiriki wenu na hatma yenu kwenye Katiba mpya. Kwa muda mrefu mmekuwa mkishawishi haki ya kupiga kura, haki ya kuwa na uraia zaidi ya mmoja (Dual Nationality) na hata namna gani mnashiriki katika kujenga uchumi wa nchi.

Kwanza nataka niwapongeze kwa kuchukua uamuzi mzito wa kuondoka nyumbani kuja ughaibuni kutafuta maisha au maarifa au vinginevyo. Nawapongeza zaidi kwa juhudi mnazofanya kusaidia familia zenu nyumbani, vijiji vyenu na hata Taifa kwa ujumla. Takwimu zilizotangazwa na Benki Kuu ya Tanzania zinaonyesha kwamba Watanzania mliopo nje ya Tanzania mlituma nyumbani fedha (remittances) zaidi ya Dola za kimarekani 350 milioni mwaka 2011. Hii ni sawa na asilimia 5 ya mapato yote ya Fedha za kigeni zilizoingia Tanzania mwaka huo na ni zaidi ya Fedha za kigeni zilizoingizwa na Chai, Kahawa, Pamba na Korosho kwa ujumla wake. Kwa hiyo ‘Diaspora’ ni sehemu muhimu sana ya Uchumi wa Taifa ni muhimu Dola iwawekee mazingira mazuri ya kuweza kufanikisha mambo yenu huku ili mshiriki vema maendeleo ya nchi yetu.

CHADEMA tunatambua umuhimu wenu hata kama msingekuwa mnatuma fedha nyumbani. Ninyi ni Watanzania na ni jukumu la Dola ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwalinda popote mlipo duniani. Mtakumbuka mwanzo mwa miaka ya 2000 kulikuwa kuna ‘petition’ ya kudai Uraia wan chi mbili kwa Watanzania. Dkt. Willibrod Slaa alikuwa ni mmoja wa Wabunge waliokuwa wanauliza maswali Bungeni kuhusu jambo hilo. Wengi tuliweka sahihi katika ‘petition’ ile ambayo ilianzishwa na Watanzania wanaoishi nje. CHADEMA inaunga mkono haki ya Watanzania kuwa na uraia wa nchi nyingine. CHADEMA inataka suala hili lifikie mwisho kwenye mjadala wa Katiba. Kuna watu wanasema sio uzalendo Mtanzania kuchukua uraia wa nchi nyingine. Ninasema sio uzalendo pia kuacha raia wako wanateseka nchi nyingine kwa sababu tu wamechukua uraia wa huko au wanashindwa kuchukua uraia wa huko. Sheri zetu za Uraia ni gandamizi hasa kwa wanawake wa Tanzania. Tumepoteza dada zetu wengi sana na watoto wao kwa sababu wakiolewa na wageni watoto wao hawana haki ya kuwa raia. Wakinyanyaswa na wageni na kutaka kurudi nyumbani wao na watoto wao wananyanyaswa pia kwao. Haikubaliki na tutakabili suala hili kwa nguvu zetu zote. Tunataka Watanzania walioko nje wapate kila aina ya msaada kutoka Dola yetu ili wafanikiwe.

CHADEMA inataka pia Watanzania waliopo nje waruhusiwe kupiga kura nyakati za uchaguzi. Ni suala la ushamba tu kuendelea kujadili jambo hili la uwazi kabisa. Kuna teknolojia za kisasa kabisa kuhakikisha watu wanapiga kura kokote walipo. Mwaka 2004 Chama rafiki cha CHADEMA kutokan Msumbiji RENAMO kiliniteua kuwa wakala wa kura katika kituo cha Ubalozi wa Tanzania Msumbiji uliopo Dar es Salaam. Raia wa Msumbiji wanaoishi Tanzania wanapiga kura nje, seuze Tanzania? CHADEMA inawahakikishia kulisimamia jambo hili.

Katika mkutano wa Bajeti ujao Bajeti Kivuli itazungumzia namna ya kuimarisha uwekezaji wa Watanzania wanaoishi nje katika uchumi wa nchi. Siku zote tunazungumzia mitaji kutoka nje kwa maana ya ‘Foreign Direct Investments’ peke yake na kwa kweli tunasahau kwamba kuna ‘Diaspora Direct Investments’. Tumetoa vivutio vingi sana kwa Wawekezaji kutoka nje. CHADEMA inakwenda kupendekeza kuwepo kwa vivutio vya kikodi na kirasimu kwa Watanzania wanaoishi nje wanaotaka kuwekeza nyumbani. Ninawashawishi muangalie namna ya kujikusanya na kuwa na ‘Investments Funds’ ili kununua ‘equties’ kwenye miradi mbalimbali. Uwekezaji Tanzania unalipa sana (Return on Investments goes up to 25%) kwenye baadhi ya maeneo. Huduma katika sekta zinazoinukia kama Mafuta na Gesi ni eneo ambalo mnapaswa kuliangalia tusiachie wageni tu. Mnakumbuka wakati wa mwanzo wa Sekta ya Madini hata huduma za kufua nilikuwa zinatolewa na kampuni kutoka Australia! Mtwara hakuna vyumba vya kutosha vya mahoteli na hata nyumba za kupanga, angalieni maeneo haya maana Mtwara is booming. Sisi kama wanasiasa jukumu letu ni kuwawekea mazingira mazuri. Ninyi mnapaswa kuzileta hizo Dola kidogo mpatazo nyumbani na kuwekeza kwenye maeneo yatakayozalisha ajira na hivyo kuondoa umasikini kwa ndugu zenu. Ninaamini mtachukua changamoto hii na kuangalia namna ya kuitekeleza. Wenzetu kutoka Ethiopia na Kenya wanafanya hivi.

Mjadala wa Katiba pia na hatimaye Katiba mpya itaamua hatma ya Muungano wetu. Muungano pekee katika Bara la Afrika ambao umedumu na umeonyesha nia ya Mwafrika kukataa mipaka ya kikoloni. Kuna Watu wanaona Muungano huu haina manufaa hivyo uvunjwe. Kuna watu wanaona ni bora kuurekebisha ili uweze kufaidisha Jamhuri mbili zilizoungana. Mchakato wa Katiba mpya kupitia Tume ya Katiba ambayo CHADEMA tumeshiriki, ni nafasi ya kuandaa mustakabali wa Tanzania ijayo. Tanzania tunayoitaka kwa miaka mingine hamsini, mia moja au hata alfu moja. Watanzania wawe huru kusema wanataka Muungano au hawautaki, wanataka Muungano wa namna gani na wanataka Tanzania ya namna gani.

Ni Haki ya Watanzania wanaoishi nje kutoa maoni yao kuhusu Katiba. CHADEMA inakusudia kwanza kukusanya maoni ya wanachama wake walioko nje kuhusu Katiba lakini pia kuitaka Tume ya Jaji Warioba kuja huku kukutana na Watanzania na kupata maoni yao. Ni Haki yenu kutoa maoni na ninawaomba mtumie haki yenu vizuri. Mtupe uzoefu wa nchi nyingine ambazo mmeishi na kuweza kuona ni vipi tutaimarisha Dola imara ya Kidemokrasia yenye kuleta ustawi wa watu wake.

Msimamo wa CHADEMA ni Muungano wa Serikali Tatu. Hata hivyo katika mchakato tulio nao sasa wanachama wa CHADEMA wana uhuru wa kutoa mawazo mapya na kuboresha sera hii ya CHADEMA kuhusu Muungano. Muwe huru kabisa kutoa maoni yenu.

Haki na Wajibu

Watanzania mnaoishi nje mna haki na lazima Dola ilinde haki hizo lakini pia kama Watanzania mna wajibu kwa nchi yenu. Ni wajibu wenu kushiriki kikamilifu katika kuimarisha demokrasia nchini. Sisi wenzenu tumejitoa muhanga katika eneo hili. Tumejenga taasisi zinazoitwa vyama vya siasa kwa zaidi ya miaka ishirini sasa. Hatuchoki lakini tunahitaji ushiriki wenu. Jambo hili sio kwa wanachama wa CHADEMA peke yake bali pia hata wanachama wa vyama vingine mnaoishi hapa Marekani.

Hutakuwa mwanachama bora wa CCM kwa kufanya kazi ya kuwachoma Watanzania wenzako ambao ni wana mageuzi kwa viongozi kila wanapokuja kwenye ziara nje ya nchi. Utakuwa mwanachama mzuri wa chama chako iwapo utawaambia viongozi ukweli wa mambo na namna bora ya kuongoza nchi yetu.

Hamuitendei haki Tanzania kwa kusemana, kusingiziana, kutetana na hata kugombana. Wakati mwingine unapoona mijadala ya watu kwenye mitandao ya kijamii unasinyaa. Unajiuliza sasa kama hawa ndio wapo kwenye mwanga sisi tulio kwenye giza inakuwaje?

Fanya kazi. Furahia maisha. Lakini kumbuka kuna nchi yenye barabara za mashimo, yenye giza muda mwingi wa mwaka kuliko mwanga, yenye umasikini, yenye viongozi wasiwajibika na wala rushwa. Ni nchi yako. Usiseme hii ni kazi ya kina Zitto, Slaa, Mbowe, Nassari, Leticia na Msigwa. Kila mtu ana wajibu wa kufanya kuisogeza mbele nchi yetu. Timiza wajibu wako kwa namna unavyoona inafaa.

Nkrumah once said ‘organise, don’t agonise’ narudia hivyo kwa Watanzania mliopo Marekani. Organise for your motherland.

Tanzania yenye usawa wa fursa

Nimalizie kwa stori yangu. Nilizaliwa katika umasikini wa kutisha kama Watanzania wengi wa vijijini. Nimekwenda shuleni bila viatu na wakati mwingi tumbo likiwa tupu ama nimekunywa uji wa unga wa Yanga uliotiwa chumvi. Darasani nilikuwa ninasoma na watoto wa watu wote wenye mamlaka pale mjini Kigoma. Wote tulikuwa tunafundishwa na Mwalimu huyo huyo na tunakaa darasa hilo hilo, tunapata elimu hiyo hiyo. Leo mimi ni msomi mwenye shahada ya Uzamili na Mbunge nawakilisha watu wa kwetu. Wenzangu wengi pia wanaendesha maisha yao na wengine wapo hapa Marekani wakitafuta maisha.

Leo mtoto wa masikini Tanzania hapati elimu anayopata mtoto wa mwenye uwezo. Mtoto wa masikini hakutani na mtoto wa mwenye uwezo. Wanasoma shule tofauti. Wanafundishwa na walimu tofauti. Hawachezi pamoja. Wote wakimaliza kidato cha Sita, mtoto wa mwenye uwezo ana nafasi kubwa zaidi ya kupata mkopo kwenda Chuo Kikuu kwa sababu amesoma shule bora zaidi hivyo anapata daraja kubwa zaidi la kupewa mkopo na Bodi ya Mikopo.

Wakati nasoma, kikwazo kilikuwa uwezo wako tu kichwani. Hivi sasa kikwazo ni kipato pia. Tofauti ya kipato nchini ni kubwa lakini sisi wanasiasa hatuioni. Wakati wenzetu wanajiandaa kufaidika na ‘demographic dividend’ kwani watoto wao wanapata elimu bora, sisi hata hatujiandai na ‘demographic Bomb’ litakaloletwa na kundi kubwa la vijana wasio na elimu wala ujuzi.

Shiriki kurejesha Tanzania yenye kutoa fursa kwa kila raia bila kujali hali yake ya kipato. Shirika kurejesha Tanzania yenye Usawa kwenye fursa na yenye demokrasia. Jiunge na CHADEMA tuendeleze mapambano.

Nawashukuru kwa kunisikiliza



Zitto Kabwe, Mb

Naibu Katibu Mkuu CHADEMA

author

This post was written by: Author Name

Your description comes here!

Get Free Email Updates to your Inbox!
© Copyright Udaku Kijiweni
Back To Top