Askofu Mkuu wa Anglican Tanzania, Dk Valontino Mokiwa wa kwanza kulia akizungumzia kuhusiana na matatizo yaliotokezea Zanzibar ya kuchomwa Moto kwa Makanisa mbalimbali huko katika Ukumbi wa Afisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar walipokutana Maaskofu mbalimbali na Waziri wa Nchi Afisi ya Makamu wa Pili wa Rais Mohammed Aboud Mohammed.
JOPO la Maaskofu wa madhehebu mbalimbali nchini jana wameitolea uvivu Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kushindwa kudhibiti vitendo vya uharibifu wa makanisa visiwani humo. Akizungumza kwa niaba ya maaskofu hao mbele ya Waziri wa Nchi Katika ofisi ya Makamu wa Pili Mohamed Aboud, Askofu mkuu wa Kanisa la Anglican Dk Valentino Mokiwa, alisema kuwa vitendo hivyo sasa vimekithiri na kwamba hawaoni Serikali hiyo ikichukua hatua madhubuti hivyo Wakristo wamechoka.
“Kanisa sasa limechoka kutokana na vitendo vya kuchumwa kwa makanisa na kuharibiwa kwa mali zake…..Leo tukirejea historia tangu mwaka 2001 kuna makanisa 25 yameshaharibiwa, yaani kuwa mkristo ni maisha ya hofu” alisema Askofu Mokiwa.
Aliongeza kuwa wakristo visiwani humo wamekuwa wakiishi kwa hofu huku wakitishiwa maish yao kwa kuopigwa mawe, huku wakichukuliwa kama daraja la pili na kwamba Serikali haichukui hatua madhubuti.
“Matukio yote hayo haya yameripotiwa polisi lakini hakuna hatua zilizochukuliwa. Tumesikiwa mkisema eti wanaofanya hivyo ni wahuni, sisi tunasema hiyo ni lugha ya kututia ganzi. Wale siyo wahuni, ni wahalifu na kuna taratubu za kuwachukuliwa kisheria. Serikali inakemea lakini haina ‘confidence’.” alisema Askofu Mokiwa.
Mokiwa pia aliitaka Serikali kueleza miakati waliyoichukuwa na kuwataja majina wahalifu waliokamatwa kwa majina ili waamini kama kweli hatua zimechukuliwa.
Aliongeza kuwa Serikali pia inapaswa kuchukua hatua kwa vikundi vya dini vinavyohubiri siasa kinyume na masharti waliopewa.
“Siyo dhambi watu kutaka nchi yao au serikali yao, lakini masuala haya hayana uhusiano wowote na muungano. Basi kuwe na majadilinao na vikundi hivi ili kuleta maridhiano.
Askofu Mokiwa alionya kwamba japo Wakristo ni wapole, wanaweza kuchukua hatua kali ili kujilinda.
“Kuna wakati tuliomba Serikali tuwe tunajilinda wenyewe na bado tunaendelea kuomba hivyo. Wakristo siku zote ni pole lakini ipo siku bubu anaweza kusema kwa mikono…. ukiona ‘yellow’ ina ‘blinc’ ujue hali ni mbaya” alionya na kuongea,
“”Ukichoma biblia kama walivyofanya unatarajia nini? Kweli tumevumilia sana lakini sasa tunaonekana wajinga.”
Mokiwa pia aliwataka viongozi wa dini zote kuhakikisha kuwa wanawaongoza waumini wao katika kutenda haki.
Akijibu malalamiko hayo Waziri Mohamed Aboud alisema kuwa atayafikisha yote kwa Rais wa Zanzibar na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania bila kupunguza hata nukta.
Alikiri kuwa Serikali imezembea katika matukio hayo lakini akasisitiza umuhimu wa viongozi wa dini kutoeneza lugha za chuki.
“Lazima tuwe na mkakati wa pamoja na kuhakikisha tunapambana na wote wanaoeneza chuki. Uvumulivu wenu mliouonyesha ni mkubwa hivyo tunaomba mwendelee. Hao wanaofanya hayo tutahakikisha tunawafikisha kwenye vyombo vya sheria.”alisema Waziri Aboud.
Akizungumzia uhusiano kati ya Wakristo na Waislamu visiwani humo, Waziri Aboud alisema tangu kanisa la kwanza lilipoanzishwa visiwani humo mwaka 1870, wamekuwa wakiishi kwa kushirikiana bila kubaguana hadi siku za hivi karibuni.
Alipoulizwa na mwandishi wa habari hizi kuhusu ukimya wa Rais wa Zanzibar Dk Ali Mohamed Shein tangu machafuko hayo yatokee, Waziri Aboud alihamaki akisema kuwa ameshatoa matamko mengi kwa nyakati tofauti.
“Rais ameshazungumza kwa nyakati tofauti, akiwa hapa na huko Pemba… ameshazungumza sana, lakini ninyi hamwandiki tu. Hata sasa amenituma nizungumze, sisi ndiyo tunaomwakilisha. Lakini ameshazungumza mno.”alijibu Waziri Aboud.
Chanzo:zanzibaryetu.wordpress.com
Loading...
Post a Comment
CodeNirvana