Featured

    Featured Posts

    Social Icons

    .
Loading...

Nassari: Sina nia ya kugawa nchi



Nassari: Sina nia ya kugawa nchi

na Waandishi wetu

MBUNGE wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari (CHADEMA), amesema kuwa hana nia wala dhamira ya kuchochea na kuhamasisha mgawanyiko katika nchi kama ambavyo imekuwa ikitafsiriwa na baadhi ya watu.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, juu ya maneno anayodaiwa kuyatoa Jumamosi kwenye mkutano wa hadhara wa chama chake wakati wa uzinduzi wa operesheni ‘vua gamba vaa gwanda’ kwenye viwanja vya NMC, Nassari alidai lengo la hotuba yake lilikuwa kuhimiza serikali na jeshi la polisi lishughulikie mauaji ya watu na kudai hakulenga kuchochea vurugu au kumzuia Rais kutekeleza wajibu wake.

“Kumetokea sintofahamu kubwa kuhusu sehemu ya hotuba yangu niliyoitoa; chama changu siku zote kimekuwa mstari wa mbele kuunganisha umma wa Watanzania wote kudai haki, umoja, amani na maendeleo ya kweli bila kujali ukanda, udini wala historia, ningependa ifahamike kuwa sina lengo wala dhamira ya kuwagawa Watanzania kwa namna yoyote ile kama ambavyo imekuwa ikitafsiriwa,” alisema Nasari.

Alisema hata kauli ya ufafanuzi iliyotolewa na Mwenyekiti wake wa Taifa, Freeman Mbowe, kwenye mkutano huo baada ya yeye kuzungumza iliweka mkazo juu ya msimamo wa CHADEMA wa kuunganisha nguvu ya umma katika maendeleo ya Watanzania.

“Hata alipohojiwa na vyombo vya usalama kutaka kujua nilimaanisha nini aliwaeleza hivyo,” alisema.

Nassari ametoa kauli hiyo siku moja baada ya jeshi la polisi kudai linasubiri ridhaa ya Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini (DPP) ili waweze kumfikisha mahakamani pamoja Mwenyekiti wa BAVICHA Taifa, John Heche, na mwanachama Ally Bananga ambaye alikuwa amehamia CHADEMA siku hiyo ya mkutano akitokea CCM alikokuwa akishika nyadhifa mbalimbali za uongozi.

Naibu Kamishina wa Polisi, Isaya Mungulu, aliwaeleza waandishi wa habari juzi kuwa baada ya kuwahoji wamebaini makosa wanayowatuhumu nayo yanaangukia katika kifungu cha sheria namba 63 b cha kanuni ya adhabu, sura namba 16 ambapo inahitaji ridhaa ya DPP kabla ya kuyafikisha mahakamani.

UVCCM wamshukia

UMOJA wa vijana wa Chama cha Mapinduzi (CCM) umemtaka Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, kuviwajibisha baadhi ya vyama ambavyo vinatumia vibaya uhuru wake.

Katibu mkuu wa umoja huo, Martin Shigela, alisema hayo jana alipokutana na wanachama wa umoja huo kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), akidai kuwa amesikitishwa na kauli iliyotolewa hivi karibuni na mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari, ya kulitaka jeshi la polisi kuwakamata waliohusika na mauaji ya wanachama wake, vinginevyo wangelijitangazia uhuru wao.

Alidai kuwa kauli ya Nassari ni ya kibaguzi na yenye lengo la kuchochea umwagaji damu, hivyo, lazima hatua zichukuliwe dhidi ya viongozi wa aina hiyo.

Aliwaambia wanavyuo hao walioandamano kwa ajili ya kumpongeza Rais Jakaya Kikwete kwa ajili ya mabadiliko ya baraza la mawaziri kuwa CCM inalaani kauli hiyo kwani siyo kauli nzuri katika mwenendo wa kisiasa.

Hata hivyo, wakati Shigela akilalama, tayari viongozi wa ngazi ya juu wa CHADEMA, wametoa maelezo kuwa huo sio msimamo wa chama chao, na Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe, alisimama na kukemea kauli hiyo.

Kwa upande wake, Nasari amedai kuwa kauli yake haikuwa na lengo baya na ililenga kuweka mabadiliko ya kihamasa katika mikoa hiyo ili wengine waone wivu wa kimaendeleo kwa mikoa ya kaskazini ambayo inaonyesha mabadiliko makubwa.

“Mimi ni mtu mdogo tu sina nguvu hata kidogo ya kutangaza uhuru huo wa sehemu yoyote ya nchi” alifafanua Nasari.

Habari hii imeandaliwa na Danson Kaijage, Hamida Ramadhani, Dodoma na Grace Macha, Arusha
author

This post was written by: Author Name

Your description comes here!

Get Free Email Updates to your Inbox!
© Copyright Udaku Kijiweni
Back To Top