Featured

    Featured Posts

    Social Icons

    .
Loading...

KUUA AMA KUUA BILA KUKUSUDIA: UCHAMBUZI MFUPI



KUUA AMA KUUA BILA KUKUSUDIA: UCHAMBUZI MFUPI
Salaam kwa wote.
Nimeonelea kutoa uchambuzi mfupi wa kawaida kuhusu jambo nililolitaja hapo juu. Uchambuzi
huu unatokana na kubaini kwamba watu wengi nilioongea nao hapa na pale juu ya kuua na kuua
bila kukusudia, wameonesha kuchanganyikiwa na maana halisi ya makosa hayo mawili.


Nikiri kwamba eneo hili ni gumu sana hasa kwa mtu wa kawaida ambaye hajapitia taaluma ya
sheria. Ni mahala panapohitaji umakini wa hali ya juu ili kuweza kuelewa juu ya maana halisi ya
makosa hayo mawili. Napenda nitoe angalizo kuwa katika uchambuzi huu sitapenda kunukuu
vifungu vya sheria kwa kirefu sana ili kurahisisha uchambuzi wangu kwa wasomaji wa kawaida.
Ila ifahamike kuwa sheria ya msingi inayoongoza makosa haya mawili ni Sheria ya Kanuni ya
Adhabu, Sura ya 16 ya Sheria za Tanzania.


Kwa ujumla, Kuua na Kuua bila ya kukusudia ni makosa ambayo mtu huyatenda dhidi ya mtu
mwingine ambayo huhesabika ni kutenda kosa dhidi ya dola. Makosa haya yanatofautiana na
makundi mengi sana kama vile makosa dhidi ya vitu, na migawanyo mingine. Sasa haya makosa
ya Kuua na Kuua bila ya kukusudia, ni makosa yaliyowekwa chini ya makosa dhidi ya
binadamu. Bila shaka ni kwa mujibu wa Kanuni ya Adhabu ya Tanzania. (Kanuni ya adhabu ni
mwongozo unaoelezea makosa mbalimbali katika Tanzania huku ikieleza adhabu inayopaswa
kutolewa kwa mtu atakayekutwa na hatia katika kosa aliloshitakiwa nalo).


Labda utajiuliza ni kwa nini tuna hiyo Sheria ya Kanuni ya Adhabu. Ndiyo, Kanuni ya Adhabu
ndiyo inayoainisha ni matendo gani yanayojenga kosa fulani na kwamba kosa hilo likithibitishwa
pasi na shaka yoyote mahakamani, basi aliyetenda kosa hilo ataadhibiwa adhabu fulani.
Tambueni kwamba Sheria ya Kanuni ya Adhabu inaainisha makosa ya Jinai tu ambayo dola
ndiyo inayoyasimamia. Ndio maana tunasema makosa ya jinai ni makosa yanayofanywa na watu
dhidi ya dola. Hii ni tofauti na mashauri ya madai ambayo huwa ni kati ya mtu na mtu mwingine.
Dhana hii ni ngumu kidogo, iweje ameuliwa Stewart kisha pasemwe kwamba dola ndiyo
iliyokosewa? Ndiyo, kwa maana dola ndiyo yenye jukumu la kulinda maisha ya watu wake na
mali zao ndiyo maana ikaweka misingi ya kisheria na kueleza mkururo wa makosa na adhabu
zake ili wenye kuogopa waogope kufanya makosa lakini almuhimu maisha ya watu na mali zao
viwe salama salimini.


Kwa kukuweka sawa zaidi, ndio maana utaona kwamba dola huwa haiingilii kati makosa yetu
tunayotendeana sisi kwa sisi kama vile kudaiana, mikataba halali iliyoparaganyika na mambo
mengine kama hayo. Tukifanyiana makosa hayo, sisi wenyewe ndio tunaiomba mahakama
(mhimili mwingine wa dola) itusaidie kutatua tatizo hilo kwani ni tatizo lililoibuka kati ya mtu
na mtu au mtu na kikundi au kikundi na kikundi. Tena huwa tunaanzia mbaaali saaana kabla ya
kufika mahakamani. Lakini kwenye makosa ya jinai, aa, hakuna sumile, ukituhumiwa tu kutenda
kosa fulani, utakamatwa, utafunguliwa mashitaka, utafikishwa mahakamani, kesi itasomwa na
kusikilizwa na mwisho hukumu itatolewa. Labda mtenda kosa aamue kujificha na asijulikane
kamwe hadi mwisho wa maisha yake. Lakini bado katika mazingira fulani shauri dhidi yake
laweza kuendeshwa pasipo yeye kuwepo mahakamani.

Bila shaka tunakwenda pamoja.

Sasa hayo makosa mawili niliyoyataja hapo juu (Kuua na Kuua bila ya kukusudia) pia ni katika
makosa ya jinai ambapo mtu yoyote atakayetuhumiwa kuyakatisha maisha ya mtu mwingine,
dola itamkamata, itamweka rumande, itamfungulia mashitaka na mwisho hukumu kutolewa.

KUUA
Kosa hili limeainishwa katika fungu la 196 la Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16. Mtu atasemekana
kuwa ametenda kosa la kuua pale itakapobainika pasi na shaka yoyote kwamba mtu huyo
alidhamiria kukatisha maisha ya mtu mwingine. Mbinu nyingi zinaweza kutumika katika kufikia
malengo hayo. Mtu anaweza akajipanga mwenyewe na kumuwinda adui yake hadi akapata
nafasi nzuri na kutimiza lengo lake la mauaji. Anaweza mtu akatumia silaha kama bunduki, kisu,
panga, gongo na vitu vingine kama hivyo. Mwingine anaweza akamtumia mtu mwingine
kutekeleza azma yake. Bila shaka ni kwa makubaliano maalum. Pia mtu anaweza akatumia
kikundi cha watu katika kufkia lengo hilo. Anaweza pia akatumia kikundi cha wataalamu wenye
uwezo wa kutotumia panga wala bunduki, lakini wakatumia mbinu za kitaalamu kama vile
matumizi ya sumu na tindikali kwa lengo hilo hilo la kuondoa maisha ya mtu. Alimuradi njia
kadhaa zinaweza zikatumika.

Adhabu ya kosa hilo litakapothibiti, ni kunyongwa hadi kufa.

KUUA BILA YA KUKUSUDIA.
Kosa hili limeainishwa katika fungu la 195 la Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16. Mtu
atasemekana kuwa ametenda kosa la Kuua bila ya kukusudia pale itakapobainika kuwa
amekatisha maisha ya mtu bila ya kuwa na dhamira ya kufanya hivyo. Kwa maana nyingine,
mauaji yamefanywa bila ya dhamira iliyoratibiwa kikamilifu ili kutenda kosa la mauaji. Hapa
napo ni pagumu maana unaweza ukajiuliza ni kwa namna gani tunaweza tukatambua kuwa
mtuhumiwa au mshitakiwa ameuwa bila ya dhamira au kukusudia kuua?

Kwa maswali hayo, tunarudi kulekule ambako inabidi wataalamu waangalie mazingira halisi ya
tukio lenyewe namna lilivyotokea. Pia wapelelezi ni budi wafanye uchunguzi wa kina ili
kujiridhisha kuwa ni kwa namna gani mtuhumiwa anaweza akawa kweli ameua bila ya
kukusudia. Lakini ikumbukwe pia kwamba ni mahakama ndiyo itakayotoa tamko kwamba huyo
mtuhumiwa ni kweli ametenda kosa hilo la kuua bila ya kukusudia. Nisisitize tena kwamba ni
jukumu la upande wa mashitaka kukusanya ushahidi wenye mashiko ambao utairidhisha
mahakama kwamba kweli mtuhumiwa ametenda kosa hilo. Pale upande wa mashitaka utakapo
wasilisha ushahidi dhaifu mbele ya mahakama, basi mtuhumiwa ataachiliwa huru.

Pale itakapothibitika kwamba mtuhumiwa kweli ametenda kosa hilo la kuua bila ya kukusudia,
ukomo wa juu wa adhabu yake huwa ni kufungwa maisha. Adhabu ndogo itategemea ni kwa
namna gani mtuhumiwa atakavyo jitetea na ni kwa namna gani mahakama itakavyopokea
maombi ya mtuhumiwa huyo na namna shauri zima lilivyoendeshwa. Adhabu hiyo inaweza
ikapunguzwa.

Labda ungependa kujua sasa ni kwa namna gani mahakama inaweza ikafikia uamuzi wa kumtia
hatiani mshitakiwa wa kosa la Kuua bila ya kukusudia. Hapa kuna mambo mengi, lakini cha
msingi ni kuangalia na kujiridhisha bila ya shaka yoyote kuhusu namna tukio lenyewe
lilivyotokea. Kwa mfano dereva aliyeingiza gari yake kwa ghafla mbele ya gari lingine na
kusababisha gari la nyuma yake kuligonga na mara madereva hao wakaacha sukani zao na
kuanza kubishana na kutukanana na kutahamaki wakarukiana maungoni huku mmoja
akimsukuma mwenziwe kwa nguvu hadi chini na kufa papo hapo, utaona kuwa hapa hakuna
aliyekuwa na dhamira ya kuua isipokuwa hali ya ghadhabu na mihemko ya mishipa ya hasira
kali zimepelekea hali ya kifo. Hivyo kwa namna yoyote ile itachukuliwa kuwa aliyeua ameuwa
bila ya kukusudia.

Pia chukua mfano wa kero ndogo ya nyumbani iliyopelekea mke kukasirika ghafla na
kumsukuma mume hadi kuangukia kwenye ncha ya meza ya kioo iliyokuwa chumbani sababu
iliyopelekea mume huyo kufariki dunia. Ni dhahiri kabisa kosa hilo litajumuishwa kuwa ni Kuua
bila ya kukusudia. Lakini ifahamike kwamba ili kufukia maamuzi hayo, mahakama ni lazima
iwe imesikiliza kwa makini mkusanyiko wa mambo mengi yaliyoelezwa mahakamani hapo na
upande wa mashitaka na ule wa utetezi.

Mnaweza mkatafakari pia inakuwaje kwa mtu aliyelewa chakari kisha akafanya jambo bila ya
kujifahamu na kusababisha kifo cha mtu mwingine. Kama itathibitika kwamba mtuhumiwa
alikuwa amelewa chakari kiasi ya kutojitambua ni kitu gani alichokuwa anafanya, basi anaweza
akaadhibiwa kwa kosa la kuua bila ya kukusudia.

Kwa upande mwingine, Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ya mwaka 1985, imetoa pia
haki ya mtuhumiwa wa kosa la mauaji ya bila kukusudia kuomba dhamana ili awe nje ya kizuizi
akisubiri kuendelea kusikilizwa kwa shauri lake hadi kutolewa hukumu. Maombi ya dhamana
yatawasilishwa mahakamani na upande wa utetezi na pindi mahakama itakaporidhika na maombi
hayo itatoa dhamana kwa mshitakiwa bila shaka dhamana hiyo itakwenda sawia na masharti
kadhaa. Mshitakiwa atakapotimiza masharti hayo ya dhamana ataachiliwa huru kwa muda kama
nilivyoeleza hapo juu.

Mwisho
Ni imani yangu kuwa sasa wale waliokuwa wanapata shida ya kutofautisha makosa haya mawili,
watakuwa wamepata uwelewa mpana zaidi. Kumbuka kwamba ni mambo ya kiufundi zaidi
yanayoangaliwa katika kumshitaki mtu aidha kwa kosa la Kuua au Kuua bila ya kukusudia.
Lakini kumbukeni kwamba kuna dhana moja kongwe katika sheria isemayo “kila mtu ni mwema
mbele ya sheria hadi pale mahakama itakapo mtia hatiani”. Maana yake ni kwamba watu wote
wanaotuhumiwa na makosa mbalimbali, bado wanatakiwa wahesabiwe kuwa ni watu wema kana
kwamba hakuna tuhuma yoyote juu yao hadi pale mahakama itakapotoa maamuzi juu ya tuhuma
zinazowakabili.

Nikipata nafasi katika katika siku zijazo kupitia uwanja huu, ninaweza nikafanyia uchambuzi wa
kina juu ya suala la dhamana. Nini maana ya dhamana, nani anapaswa kupewa dhamana, ni nani
anayetoa dhamana na ni makosa yepi mtuhumiwa anaweza akapewa dhamana. Lakini je mtu
anaweza akakataliwa dhamana hata kama kosa alilotenda linadhaminika?

Nawashukuruni na Allah awabariki.

Imetayarishwa na:
Ndugu Maulana Ayoub Ali
Kitivo cha sheria, Chuo Kikuu Huria cha Tanzania
Makao Makuu, Dar Es salaam.
+255 713 046 591
libila@yahoo.com, maulana.ayoub@out.ac.tz
Imehaririwa na ndugu Alex B. Makulilo akiwa Ughaibuni, Ujarumani.
author

This post was written by: Author Name

Your description comes here!

Get Free Email Updates to your Inbox!
© Copyright Udaku Kijiweni
Back To Top