Featured

    Featured Posts

    Social Icons

    .
Loading...

TAMKO LA MHE. DR. TEREZYA L. HUVISA (MB), WAZIRI WA NCHI OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MAZINGIRA) KUHUSU SIKU YA KUPAMBANA NA KUENEA KWA HALI YA JANGWA NA UKAME DUNIANI


Ndugu Wananchi,

Mtakumbuka kuwa tarehe 17 mwezi Juni kila mwaka, duniani kote huadhimishwa Siku ya Kupambana na Kuenea kwa Hali ya Jangwa na Ukame (World Day to Combat Desertification). Mwaka 1994 Baraza la Umoja wa Mataifa lilitangaza tarehe 17 mwezi Juni ya kila mwaka kuwa ya maadhimisho ya siku hii. Lengo kuu la kuadhimisha siku hii ni kukuza
weledi miongoni mwa jamii juu ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Kupambana na Kuenea kwa Hali ya Jangwa na Ukame na utekelezaji wake duniani, hususan katika nchi zilizoathirika zaidi na tatizo hili na hasa katika bara la Afrika.

Ndugu Wananchi,

Kauli mbiu ya mwaka huu 2012 katika kuadhimisha siku ya Kupambana na Kuenea kwa Hali ya Jangwa na Ukame inasema “Udongo wenye rutuba hulinda maisha yako: SHIME TUEPUKE UHARIBIFU WA ARDHI”. Kauli mbiu hii inadhihirisha umuhimu wa kuhifadhi na kusimamia matumizi endelevu ya ardhi ili kuleta ustawi wa jamii hasa kupitia shughuli za kilimo.

Takwimu zinaonesha kuwa robo ya dunia ambayo ni zaidi ya hekta bilioni 3.6 zinatishiwa na janga la kuenea kwa hali ya jangwa na ukame. Tatizo hili linasababisha matatizo ya kiuchumi, kijamii na kimazingira kwa zaidi ya watu milioni 900 duniani. Maeneo kame ndiyo yanayotoa picha kamili ya uhaba wa chakula duniani kutokana na ukame kuathiri uwezo wa ardhi
kuzalisha. Watu zaidi ya bilioni 2 duniani wanaishi katika maeneo kame ambako ndiko pia umasikini ulikokithiri . Kwa upande wa bara la Afrika, kuenea kwa hali ya jangwa na ukame ni tatizo sugu katika maeneo kame ambapo limeathiri asilimia 73 ya maeneo haya. Hali hii imepunguza uwezo wa ardhi kuzalisha mazao ya chakula na hivyo kuongezeka kwa tatizo la
njaa na upungufu wa chakula wa mara kwa mara. Aidha, katika maeneo

haya upatikanaji wa maji ni tatizo kubwa hivyo kuathiri ustawi wa jamii, maisha ya mifugo na wanyama wa porini kwa ujumla.

Ndugu Wananchi,

Tatizo la kuenea kwa hali ya jangwa na ukame ni kubwa pia hapa nchini Tanzania. Inakadiriwa kuwa kiasi cha asilimia 45 hadi 75 ya nchi yetu ni eneo kame na linakabiliwa na tatizo hili. Maeneo ya katikati ya nchi ikiwa ni pamoja na mikoa ya Dodoma na Singida; na baadhi ya sehemu katika mikoa ya Mwanza, Shinyanga, Mara, Iringa, Manyara na Arusha
yameathirika kwa kiwango kikubwa.

Wote tunajua kuwa ardhi ni chanzo kikuu cha bidhaa na huduma mbalimbali ikiwa ni pamoja na chakula, maji safi, nishati na makazi. Ardhi pia ni chanzo kikubwa cha kipato kutokana na shughuli za kilimo, uvuvi, misitu na utalii. Theluthi mbili ya utajiri wa Tanzania unategemea rasilimali asilia za ardhi. Sekta ya kilimo ambayo inategemea sana uzalishaji kutokana na ardhi hususan ardhi ya kilimo, inachangia asilimia 45 ya pato la Taifa (GDP) na asilimia 50 ya fedha za kigeni. Aidha, sekta ya kilimo inatoa ajira kwa asilimia 80 ya watanzania
waishio vijijini na kuchangia kwa zaidi ya asilimia 90 ya mahitaji ya chakula kwa taifa.

Ndugu Wananchi,

Ni ukweli usiopingika kuwa mabadiliko ya tabianchi yanaleta athari nyingi ikiwemo kuenea kwa jangwa na ukame. Adhari hizi ndio zinazokwamisha juhudi zetu kama nchi za kuondoa umaskini na kufikia malengo ya Milenia. Hata hivyo nchi kama Tanzania ambayo uchumi wake kwa kiasi kikubwa unategemea ubora wa ardhi, suala la ardhi yenye rutuba lina umuhimu wa pekee.

Tunaamini kuwa matumizi endelevu ya ardhi ndiyo yatakayotuwezesha kuhimili na kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi. Inatupasa sasa tutambue uhusiano uliopo kati ya changamoto hizi na umuhimu wa kufanya juhudi zenye uwiano linganifu ili kukabiliana
na changamoto hizi zote. Kutokana na umuhimu wa ardhi katika maisha na ustawi wa jamii duniani, tunatakiwa kuweka lengo la kutoruhusu uharibifu wa ardhi. Lengo hili litafikiwa iwapo jamii itazingatia matumizi endelevu ya ardhi na kutumia kilimo kinachozingatia hifadhi ya ardhi.

Aidha, juhudi
zielekezwe katika kuongoa maeneo yote yaliyoharibika na kuyahifadhi yale ambayo yanatishiwa na uharibifu wa ardhi. Kipaumbele kiwekwe katika maeneo kame ambayo ni tegemeo katika uzalishaji wa chakula duniani. Maeneo haya kame kwa sasa hayako salama kutokana na tatizo la kuenea kwa hali ya jangwa na ukame; na uzalishaji wa chakula unazidi kupungua mwaka hadi mwaka.

Ndugu Wananchi,

Kwa kumalizia naomba niwakumbushe kuwa kilimo ndiyo uti wa mgongo wa uchumi wa taifa letu. Kwa sababu hii, kauli mbiu ya mwaka huu 2012 “Udongo wenye rutuba hulinda maisha yako: SHIME TUEPUKE UHARIBIFU WA ARDHI ” inatukumbusha umuhimu wa kuitumia vizuri ardhi tuliyojaliwa ili itusaidie katika kupiga vita umasikini na kutuletea maendeleo endelevu. Napenda kutumia fursa hii kuviomba vyombo vya habari kuhamasisha na kuelimisha jamii juu ya umuhimu wa kuchukua hatua muafaka kupambana na kuenea kwa hali ya jangwa na ukame.


Vyombo vya habari vina nafasi kubwa na ya kipekee katika kufanikisha hili na naamini vitasaidia. Aidha, napenda kutumia fursa hii kuhimiza sekta binafsi kuongeza uwekezaji katika kilimo na matumizi endelevu ya ardhi. Kwa kufanya hivi, tunaamini kuwa sekta hii itachangia katika kuinua maisha ya watanzania na kuondokana na umasikini hususan katika maeneo kame nchini.

Dk. Terezya L. Huvisa (MB)

WAZIRI WA NCHI – OFISI YA MAKAMU WA RAIS – MAZINGIRA

17 Juni, 2012.
Email This BlogThis! Share to Twitter Share to Facebook
author

This post was written by: Author Name

Your description comes here!

Get Free Email Updates to your Inbox!
© Copyright 2025 Udaku Kijiweni | Designed By Code Nirvana
Back To Top