Featured

    Featured Posts

    Social Icons

    .
Loading...

TFF: Yondani mchezaji huru


Kalunde Jamal
SHIRIKISHO la Soka la Tanzania, TFF limemaliza utata uliopo juu ya uhamisho wa Kelvin Yondani kwa kusema mchezaji huyo alimaliza mkataba wake na Simba, Mei 30 mwaka huu na hawana taarifa zozote juu ya usajili wake wa sasa unaoendelea.

Kauli hiyo ya TFF imekuja baada ya klabu za Simba na Yanga kudai zimemsajili beki huyo tangu mwishoni mwa mwaka jana.

Akizungumza na Mwananachi, Mkurugenzi wa mashindano wa TFF, Sadi Kawemba alisema dirisha la usajili limefunguliwa Juni Mosi na yeye ataanza kupokea taarifa za uhamisho wa wachezaji pamoja na suala la mikataba yao kuanzia Juni 15.

Alisema hivi sasa hajapokea taarifa zozote kuhusu Yondani kusaini mkataba wa miaka miwili Simba tangu mwaka jana wala Yanga ambao hajui wamesaini naye mkataba lini.

"Ninachoweza kusema ni kwamba sina taarifa hizo ninachojua ni kwamba nitaanza kupokea makubaliano ya mikataba kuanzia Juni 15, hivyo atakayeleta kabla ya hapo utakuwa batili," alisema Kawemba.

Awali Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage aliwaambia Waandishi wa habari kuwa kutokana na kitendo walichofanya Yanga cha kuamua kumsajili mchezaji ambaye tayari ana mkataba atawachukulia hatua ya kuwashtaki katika Shirikisho la Soka Duniani FIFA.

Alisema mkataba wa awali wa Yondani ulimalizika Mei 31, 2012, lakini wao waliingia naye mkataba mwingine mwaka jana mwezi Desemba 23 ambao utadumu kwa miaka miwili hadi Mei 31, 2014.

"Nimewatuma mawakili wangu na watakaa leo (jana) kulijadili suala hilo kabla ya kupeleka kesi Fifa kwani kanuni za TFF zinaniruhusu kwenda moja kwa moja FIFA kama hakuna kifungu cha sheria kuhusiana na jambo lililoleta utata, nitafanya hivyo,"alisema Rage.

Alisema,"tumejiandaa kuishtaki Yanga katika chombo husika cha mpira na kudai adhabu ya kutopitisha majina yote ya usajili ya Yanga kwa mwaka 2012/2013 na miaka mingine miwili ijayo."

Aidha Rage aliongeza kuwa wanapeleka malalamiko TFF kuhusiana na mchezaji wao Yondani kuchukuliwa na Yanga kwenye kambi ya timu ya Taifa bila ruhusa yao.

Alifafanua kuwa kuhusiana na taarifa kuwa Yanga walimsaini Yondani siku nyingi sio kweli kwa kuwa hata nguo aliyovaa wakati anasaini mkataba huo ni jezi zilizotolewa na Kampuni ya Bia TBL mwezi uliopita walipoingia mkataba mpya na TFF.

Naye msemaji wa Yanga, Louis Sendeu alisema Yondani ni mali yao kwani waliingia naye mkataba tangu mwezi Februari 20 mwaka huu.

Sendeu alisema kuwa wamefuata taratibu zote za Fifa za kumsajili mchezaji huyo ikiwamo kuongea naye miezi sita kabla ya ligi kumalizika.

"Hatukubali kuyumbishwa na vitisho vya uongozi wa Simba kwa kuwa sheria zote tunazifahamu na tukigundua kuna udanganyifu wowote umefanyika basi tutachukua hatua kali za kisheria bila kujali hadhi ya mtu,"alisema Sendeu.

Hii sio mara ya kwanza kwa Simba na Yanga kukubali kutapeliwa baada ya mchezaji kusajili timu hizo mbili na kupokea fedha kwani ilikuwa hivyo kwa Victor Costa, Kenneth Mkapa, Mohamed Mwameja na sasa Yondani.
Source:Mwananchi.
author

This post was written by: Author Name

Your description comes here!

Get Free Email Updates to your Inbox!
© Copyright Udaku Kijiweni
Back To Top