Kama vile mmea unavyoweza kupandwa kwenye mbolea ukaota, kukua na
baadaye kuzongwa na magugu ambayo huudumaza na hatimaye kama
hayatang’olewa kuua, ndivyo ndoto za mwanadamu na mafanikio yanayoweza
kujengewa tabia njema ya kukua lakini baadaye tabia mbaya ambazo huja na
mafanikio zikaua kila kitu.
Ili mwanadamu afanikiwe maishani mwake ni lazima awe na tabia pamoja
na mwenendo unaovuta au kuchochea mafanikio, zipo tabia za namna hiyo
maishani ambazo mwanadamu akizifanya na kuzifanya ziwe sehemu ya maisha
yake, mafanikio humfuata hata kama hayataki! Lakini ziko tabia ambazo
mwanadamu anaweza kuzianzisha maishani mwake, zikaota mizizi na kuwa
sehemu yake, ambazo hukwamisha kabisa mafanikio na hata kama kuna kipaji
zinaweza kukiua kisimletee manufaa yoyote maishani.
Wapo watu wengi waliozaliwa na vipaji vya kuimba, kuandika, kucheza
mpira na kadhalika lakini kwa sababu ya tabia fulani walizozianzisha
maishani mwao, vipaji hivyo vilikufa kama ambavyo mmea hufa ukizongwa na
magugu.
Tabia mbaya zinatesa watu, zimerudisha watu nyuma, zimefanya watu
waliotakiwa kuwa mabilionea wafe wakiwa maskini, waliotakiwa kuandika
vitabu au kugundua dawa za kutibu magonjwa, walikufa bila kufahamu
kwamba hiyo ndiyo ilitakiwa kuwa hatima yao kwa sababu ya tabia mbaya ya
hofu.
Tabia zote mbaya na nzuri hujengwa, hakuna mwanadamu aliyezaliwa na
tabia mbaya au nzuri, zote tumezitengeneza sisi wenyewe wakati tunakua,
nazo baadaye hugeuka kuwa vichocheo au vigingi vya sisi kuelekea kwenye
mafanikio! Kila mwanamke anapozaa mtoto, watu husema tu “mama fulani
amezaa mtoto wa kike au wa kiume!” Hakuna mwanamke hata mmoja ambaye
huzaa halafu watu wakasema “leo mama fulani amezaa jambazi” au “mama
fulani amezaa mteja wa unga!” au “mama fulani amezaa mzinzi!” wanawake
wote huzaa watoto wazuri wanaovutia, lakini watoto hawa ukiwafuatilia
baadaye maishani mwao huishia kuwa na tabia fulani ambazo hawakuzaliwa
nazo, bali walijifunza wakati wanakua.
Ziko tabia zinazochochea maendeleo au kuvuta mafanikio kumfuata mtu,
ukiwaangalia watu wengi waliofanikiwa maishani huwa na tabia za kufanana
na miongoni mwa tabia hizo ni; UADILIFU, UAMINIFU, USEMA KWELI, DHAMIRA
NA UCHAPAKAZI NA HOFU YA MUNGU.Mtu mwadilifu na mwaminifu huwavuta watu
wengi sana kufanya naye kazi, watu wengi wanataka kuhusiana na watu
waaminifu na waadilifu badala ya matapeli na watu waongo wasiosema
ukweli! Vilevile watu wavivu wasio na dhamira ya kufanikiwa na hata
wasio na hofu ya Mungu, huvuta watu wachache sana kushirikiana
Watu wengi wenye tabia mbaya hujitenga wao wenyewe au kutengwa na
jamii bila kufahamu, kwa sababu hiyo bahati ambazo siku zote maishani
mwetu huletwa na watu huwa haziwafikii kirahisi kwa sababu sifa zao
mbaya huwa zimesambaa! Hivyo basi mwanadamu anaweza kuwa hana fedha,
lakini sifa yake ya uadilifu na uaminifu ikamfanya aungane na mtu mwenye
fedha anayetafuta watu wa kushirikiana nao, ndiyo maana kuna msemo
usemao uaminifu ni mtaji.
Kama tunataka kufanikiwa maishani ni vizuri sana kujiepusha na tabia
mbaya ambazo tumezitengeneza wenyewe maishani mwetu na zimegeuka kuwa
vikwazo au vigingi kwenye maendeleo, tabia hizi zipo, lazima ziondolewe
kama kweli mtu amedhamiria kubadilisha maisha yake.
Hakuna mwanadamu aliyekamilika kila mmoja wetu analo eneo fulani
maishani mwake ambalo anapambana ili awe bora, hivyo basi kama unafahamu
tatizo lako ni matumizi mabaya ya fedha au ulevi au uzinzi au matumizi
ya dawa za kulevya, tabia ambazo zimekukwamisha kusonga mbele ni lazima
uziue tabia hizo mara moja ili upate kufanikiwa.
Ni kweli ni kazi ngumu sana kuua tabia ambayo umeijenga kwa muda
mrefu, lakini inawezekana kabisa kufanya hivyo, utaumia lakini baadaye
utasikia furaha! Si lazima uikate tabia hiyo mara moja, unaweza
kupunguza kila siku hatimaye ukakata mizizi yake kabisa.
Mfano kama unakunywa bia ishirini kila siku na hizo ndizo
zinazomaliza fedha zako ambazo ungezitumia kujenga nyumba au kuwekeza,
unaweza kupunguza bia mbilimbili kila siku hatimaye siku moja utajikuta
hujanywa bia kabisa na kuendelea na maisha hayo.
Wakati unapunguza bia unakuwa na jambo jema unalolianzisha kwa ajili
ya kuchukua nafasi ya bia huku ukiwaepuka marafiki ambao siku zote
walikuchochea kuendelea na tabia hiyo. Haya yakifanyika unaweza kung’oa
tabia zote mbaya katika maisha yako na kuanzisha tabia njema
zitakazokuwezesha kusonga mbele.
SOURCE:GPL