JUZIJUZI
nilirudi kijijini kwetu kwenda kuwaona wazazi, na pia kushtaki kwani
mambo kazini yalikuwa hayaendi sawasawa kabisa. Si unajua tena ukirudi
kijijini kuna mambo mengi yanahusika.
Tena kama babu yako mzaa baba au mama
yupo hai ukimwelezea matatizo yanayokukabili mjini, kama ni Wakristo
watakuombea na kama ni Waislamu watafanya dua.
Pia kama ni wapagani watakufanyia mambo
ya jadi au kukupeleka kwa mtaalam ili mjukuu wao uondokane na mikosi
inayokufanya mambo yako yasikuendee vizuri, kisha watakwambia rudi mjini
kila kitu kitakwenda sawa.
Basi siku ya kwanza unapofika kijijini
ni salamu na kutembelea ndugu, japo unapewa masharti nani umtembelee na
nani usikanyage kwake, hii inatokana na wanakijiji kujuana vizuri, kuwa
kuna watu wengine ukiwasalimu tu na kama hujajitengeneza basi ndo ujue
mikosi inakufuatia.
Siku ya tatu ndiyo ikawa ya kuanza
shughuli za kujitengeneza, maana baada ya kuwaambia wazee kuwa mjini
nafanya kazi lakini hela sijui inaenda wapi, ikakubalika lazima kuna
mkono wa mtu.
Pia baada ya kulinganishwa na wenzangu
ambao tulimaliza la saba wote, ikaonekana mimi tu ndiyo sina kitu, hata
mke wala mtoto sina, ni wazi kulikuwa na kitu kinaziba nyota yangu.
Baada ya wazazi wangu ambao wanapenda
sana mambo ya kishirikina kushauriana ni mtaalam yupi angefaa kuniwekea
mambo yangu sawa, wakakubaliana wanipeleke kwa mmoja aliyekuwa anaishi
kijiji cha jirani.
Basi nikapelekwa kwa mtaalam huyo
ambaye alipoangalia nyota ikagunduliwa kuwa kumbe pale kazini kwangu
kuna jamaa wamechafua nyota yangu.
Hili liliniuma sana, mi mpiga debe
stendi ya mabasi, washkaji wote nilijua rafiki zangu kumbe kuna wabaya
wangu nacheka nao palepale kijiweni, dah roho iliniuma sana, nilimuomba
mtaalam kama ikiwezekana mbaya wangu akutwe na mabaya zaidi, lakini
mtaalam akasema hiyo siyo lazima, ila nikifika tu nitamjua mbaya wangu.
Basi mtaalam akanitengeneza, kisawasawa,
chale mwili mzima, akanipa na hirizi kubwa, siku hizi watoto wa mjini
wanaiita Pawa Benki, nikaruhusiwa kurudi kazini.
Baba akalipa mbuzi mweusi mwenye doa
jeupe nikaruhusiwa kurudi mjini. Kiukweli wakati narudi furaha ilikuwa
imenijaa moyoni, maana niliambiwa mbaya wangu nitamjua na
atakayenijaribu kila kitu kitamrudia mwenyewe.
Leo nimemaliza mwezi, mbaya wangu
sijamjua, na hela ngumu kama mwanzo. Nafikiria kurudi kijijini
tukanyang’anye yule mbuzi nimuuze, japo nipate hela ya siku mbili tatu.