KWENU warembo wa Bongo Movies, Wema
Sepetu ‘Madam’ na Kajala Masanja. Habari zenu binafsi? Bila shaka ni
wazima wa afya na mnaendelea na majukumu yenu ya kila siku. Kitambo
kidogo sijawaona lakini naamini pumzi ya bure mnaendelea kuivuta ndiyo
maana nasikia matukio yenu kwenye vyombo vya habari.
Mkitaka kujua afya yangu, mimi ni mzima.
Namshukuru Mungu naendelea na shughuli zangu kama kawaida. Mungu ni
mwema sana, anaendelea kubariki kazi ya mikono yangu, namuomba yeye
aendelee kunibariki zaidi na zaidi.
Dhumuni la kuwaandikia barua hii ni
kutaka kuwakumbusha kwamba nyinyi kwa sasa ni watu wazima. Umri wenu
unatosha kabisa kusema haufanani na yale matukio yasiyokuwa na kichwa
wala miguu. Mara kadhaa nimewahi kuwaambia, hata yale mashindano yenu ya
kumwaga fedha ukumbini, nyakati hizi si zake.
Mambo ya kuibiana mabwana kama
yalishatokea, itoshe sasa kusema ulikuwa ni ujana. Kwa kuwa ilitokea,
hakuna namna zaidi ya kuyasahau na kuchapakazi. Soko lenu la filamu bado
haliridhishi, lakini mnapaswa kukomaa ili angalau mtengeneze fedha
kupitia kazi zenu na si kuhongwa.
Binafsi sikufurahishwa na tukio lenu la
kukutana ukumbini na kuzinguana mbele ya kadamnasi lililoripotiwa wiki
iliyopita na magazeti Pendwa. Lilikuwa tukio linaloonesha kwamba bado
hamjakua kitu ambacho sitaki kukiamini.
Wema Sepetu ‘Madam’.
Kama nilivyotangulia kusema hapo awali,
huu siyo wakati wa nyinyi kuoneshana ubabe wa fedha. Kwamba eti kwa kuwa
mwenzako kaenda kutunza msanii jukwaani, na wewe lazima utunze nyingi
zaidi ili uonekane wewe ni zaidi.
Ndugu zangu, bahati nzuri maisha yetu
tunajuana. Kwa kiasi kikubwa natambua maisha ya wasanii wetu nchini
hususan warembo. Wengi wenu hamtegemei sanaa kuendesha maisha yenu.
Wengi mnategemea mapedeshee au ‘mabwana’ kutamba mjini.
Niwashauri hizo fedha mnazozipata ni
bora mngewekeza kwenye sanaa yenu. Mkajizatiti vizuri ili ziweze
kuzaliana. Mnapigana ili iweje? Mnatambiana mbele za watu inawasaidia
nini. Wenzenu wanapigana siku hizi wanaingiza fedha.
Nyinyi kazi yenu si ubondia. Kazi yenu
ni uigizaji. Igizeni kwelikweli na Watanzania wawaunge mkono kwa kununua
kazi zenu. Sanaa yenu ina changamoto nyingi, mnawezaje kuzishughulikia
ikiwa hamna umoja.
Mtawezaje kutatua changamoto hizo ikiwa
hamna upendo kati yenu? Si rahisi kutatua changamoto hizo wakati mna
chuki. Ili mfanikiwe, mnahitaji kushirikiana. Shirikianeni ili muweze
kuisogeza sanaa mbele, acheni vita ya kipuuzi mnayoendelea kuifanya.
Mkizingatia hayo niliyowaambia, hakika
tutaona mabadiliko kwenu na sanaa kwa ujumla. Nina imani nyinyi ni watu
wazima na mtajipanga upya na mtaanza kuchapa kazi kama kauli mbiu ya
rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Joseph Magufuli,
‘Hapa Kazi Tu’.
Ni mimi mtu wenu,
Erick Evarist.
KWA NAFASI ZA KAZI BOFYA HAPA >>>>>>>
KWA WANAFUNZI PATA MATERIAL HAPA>>>>>>>>>>>