Yule mfanyabiashara mkubwa jijini Dar es Salaam mwenye hadhi ya kigogo,
Daudi Yakubu Adam ‘Daudi Kanyau’ (46) ambaye jana gazeti dada na hili,
Uwazi liliandika habari yake akilidai gazeti hilo Sh. Milioni 500 kwa
madai lilimchafua, ameburuzwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu,
Dar Jumatano iliyopita akituhumiwa kwa mambo mawili.
MASHITAKA YAKE YAKO HIVI
Mbele ya hakimu mkazi wa mahakama hiyo, Thomas Simba, Kanyau ambaye ni
mkazi wa Salasala, Dar alisomewa mashitaka ya kujipatia mali
zinazodhaniwa kuibwa au kupatikana kwa njia isiyo halali.
Kanyau aliambiwa mahakamani hapo kuwa, makosa hayo yapo kinyume cha sheria namba 16, kifungu cha 312 (1) (b) ya mwaka 2002.
“Kesi hii namba 17/ 2016 naiahirisha hadi Februari 17, mwaka huu na
mtuhimwa utaendelea kuwa nje kwa dhamana, “ alisema Hakimu Simba.
AWAPIGA MKWARA WAANDISHI
Wakati anatoka mahakamani, mtuhumiwa huyo alikuwa akiwazuia waandishi wa
gazeti hili kumfotoa. Hata hivyo, juhudi zake hazikuzaa matunda.
KABLA YA KIZIMBANI
Kanyau alipandishwa kizimbani baada ya kushikiliwa kwa siku 7 na Polisi
wa Kitengo cha Kuzuia na Kupambana na Madawa ya Kulevya, Makao Makuu,
Kurasini jijini Dar es Salaam na habari za kukamatwa kwake kuandikwa na
gazeti dada na hili, Uwazi la Januari 19, mwaka huu.
Gazeti la Uwazi liliripoti kukamatwa kwake.
KANYAU ACHARUKA
Mara baada ya habari hiyo kuandikwa gazetini, Kanyau kupitia kwa
mawakili wa Kampuni ya Brocard Attorneys ya jijini Dar, wiki iliyopita,
waliliandikia barua Gazeti la Uwazi akilidai fidia ya Shilingi
500,000,000 kwa madai kuwa, habari ile ilikuwa ni ya uongo kwani mteja
wao hajawahi kutuhumiwa, kukamatwa na polisi wala kufikishwa mahakamani.
KAMANDA WA KIKOSI CHA KUZUIA MADAWA YA KULEVYA
Baada ya Uwazi kupata barua hiyo kutoka kwa watu ambao Kanyau anawaamini
ni wanasheria, Februari 2, mwaka huu, waandishi wetu walikwenda Makao
Makuu ya Kikosi cha Kuzuia na Kupambana na Madawa ya Kulevya Tanzania na
kuonana na mkuu wa kitengo hicho, DCP Robert Boaz (mrithi wa Geofrey
Nzowa) ambaye alithibitisha kikosi chake kumkamata Kanyau.
“Siyo tu kwamba tumemkamata, tayari tumeshamfikisha katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.”
Akanyanyua simu yake ya mkononi, akaongea na upande wa pili kuulizia kuhusu kesi hiyo kisha akakakata na kuendelea kusema:
“Haya! Kumbe kesi yake itatajwa tena kesho Jumatano (Februari 3, mwaka huu).”
Kamanda Boaz alisema kikosi chake kinapomkamata mtu na kumhoji,
humpeleleza mambo mengi na wakipata uthibitisho humpeleka mahakamani ili
sheria ifuate mkondo wake.
WAZIRI KITWANGA AKAZIA MADAI
Katika kudhihirisha kuwa, kweli Kanyau alishikiliwa na ‘polisi wa kuzuia
unga’, hivi karibuni, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles
Kitwanga akizungumzia hali ya madawa ya kulevya nchini, aliliambia
Gazeti la Raia Mwema jinsi kikosi cha kuzuia na kupambana na madawa ya
kulevya kilivyomkamata Daudi Kanyau kwa madai ya ‘unga’.
NUKUU YA WAZIRI KITWANGA KUHUSU ‘UNGA’
“Nimeagiza wakuu wa upelelezi kote nchini waunde timu za kupambana na
madawa ya kulevya maana tumekamata mengi sana na hiyo si nguvu ya soda,
labda mimi nifukuzwe hapa (uwaziri).
“Nimeagiza watendaji wa polisi na uhamiaji na idara nyingine wanipatie
taarifa Ijumaa ya kila wiki. Ninafahamu mtandao wote, ndiyo maana
nilisema sihitaji orodha bali nahitaji kufanya kazi ili watu wanaofanya
hizi biashara wafikishwe mahakamani.
“Mfano ni namna kikosi changu (dhidi ya madawa ya kulevya) kilivyomtia
nguvuni Daud Kanyau, anayedaiwa kujihusisha na biashara hizo.“Wewe mtu
kama Kanyau alikuwa anakamatika? Ninachohitaji ni ulinzi. Kuwa
‘protected’. Mungu akihitaji ufe leo utakufa saa hiyohiyo lakini
akihitaji kukutumia kwa ajili ya watu wake atakutumia, hata kwenye
vitabu vitakatifu imeandikwa,” mwisho wa nukuu ya Waziri Kitwanga na
gazeti hilo la Februari 3, mwaka huu.
MASWALI KWA KANYAU
Kama kweli Kanyau hakukamatwa kama mawikili wake walivyosema, Waziri
Kitwanga alikuwa akimzungumzia Kanyau gani?!Kama kweli hajatuhumiwa
chochote, kule mahabusu ya Polisi Ufundi iliyopo Kilwa Road kwenye
kitengo cha kupambana na madawa ya kulevya, alikaa kwa siku saba kwa
sababu gani?!
KUTOKA MEZANI KWA MHARIRI
Tunapenda kuwaambia wasomaji wetu kwamba, habari ambazo zimekuwa
zikiandikwa na Magazeti Pendwa ya Global Publishers (Risasi Jumatano,
Amani, Ijumaa, Risasi Jumamosi, Ijumaa Wikienda, Uwazi pamoja na ya
michezo, Championi), ni za uhakika na ukweli mtupu zikiwa zimefanyiwa
uchunguzi wa kutosha.