Loading...
Sugu, Kikombe cha Chai na Maandazi
Mh.Joseph Mbilinyi a.k.a Sugu.
Sugu awa kivutio Mbeya
WAKATI mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi (CHADEMA), akianza kazi katika mazingira magumu, baada ya kukabidhiwa ofisi isiyo na samani, juzi aligeuka kivutio kutokana na uamuzi wake wa kwenda kunywa chai eneo ambalo hutumiwa na watu wa kipato cha chini maarufu ‘Mwiboma’.
Akiwa ameambatana na madiwani wa chama hicho, Mbilinyi maarufu kwa jina la Sugu, alifika katika eneo hilo ambalo ni sehemu ya Soko la Uhindi lililoteketea kwa moto na kuagiza chai ya rangi na maandazi, jambo ambalo lilifanya mama na baba ntilie, pamoja na wateja waliokuwepo eneo hilo kugeuza ujio wa mbunge huyo kuwa mkutano.
Tukio hilo lililoelezewa na wafanyabiashara kuwa ni ujasiri na lenye kulenga kuwa karibu zaidi na wananchi kwa lengo la kubaini kero na matatizo yao kwa ukaribu lilitokea muda mfupi baada ya kumalizika kwa semina ya madiwani iliyofanyika katika ukumbi wa halmashauri ya Jiji la Mbeya.
Akiwa na kundi la madiwani wa CHADEMA, walifika sokoni hapo na kwenda moja kwa moja katika meza za wateja na kuanza kuagiza chai na maandazi, hali iliyowafanya baadhi ya mama ntilie kusita kutoa huduma.
Baadhi ya wafanyabiashara waliomtambua mbunge huyo, walianza kusambaza ujumbe kwa wenzao waliokuwa jirani na kusababisha mkusanyiko mkubwa eneo hilo, hali iliyogeuza ujio huo wa kifungua kinywa kwa mbunge na madiwani kuwa kama mkutano ambapo wafanyabiashara hao walianza kueleza matatizo na kero.
“Hii ni kali yaani mheshimiwa leo kaamua kuja kunywa chai benchini, sijawahi kuona viongozi kama hawa ndo wanatakiwa, badala ya kujichimbia mbali hali inayofanya kushindwa kutambua matatizo ya wananchi,” alisikika mmoja wa wafanyabiashara hao.
Waliongeza kuwa kitendo kilichofanywa na mbunge huyo kimeweka rekodi kwa kuwa hakuna mtangulizi wake hata mmoja wa nafasi hiyo aliyethubutu kwenda kunywa chai eneo hilo na kwamba hata mbunge mstaafu wa jimbo hilo, Benson Mpesya, hakuwahi kufanya hivyo licha ya awali kufanya biashara hapo.
“Mwiboma ndiko alikoanzia maisha Mpesya, lakini tangu alipopata ubunge miaka kumi hakuwahi kufika eneo hilo alilofanyia biashara kipindi cha nyuma,” alipasha mfanyabiasha mmoja.
Kwa upande wake, Mbilinyi alisema lengo la kwenda kunywa chai Mwiboma halikuwa la kikazi bali waliamua kwenda kufungua kinywa eneo hilo kwa kuwa linakidhi haja na si kwa ajili ya watu fulani tu.
“Ndugu yangu hili ni eneo safi sana, kila kitu kinapatikana si unaona, mimi sijaja kutania hapa nakunywa chai na maandazi,” alisema Mbilinyi.
Chanzo Tanzania Daima.
Picha kwa Hisani ya Full Shangwe Blog.
Post a Comment
CodeNirvana