Ndugu yangu
Mjengwa
Mawazo yako yamenigusa sana. Uliyoyatafakari baada ya kushuhudia
uliyo yashhudia Iringa ni mambo wengine tumeanza kuyatafakari kwa kitambo kidogo
hususani tangu Chama cha Chadema kilipomtangaza Dr. Slaa kuwa ngombea wake wa
kiti cha Uraisi katika Uchaguzi Mkuu mwaka jana. Wewe umesema hivi: "Nimeishi
Iringa kwa miaka saba sasa. Nikiri, kuwa sijapata kushuhudia maandamano makubwa
ya wafuasi wa chama cha siasa kama yale ya CHADEMA Alhamisi iliyopita. Sijapata
pia kushuhudia mkutano mkubwa wa chama cha siasa kama ule wa CHADEMA pale
viwanja vya Mlandege" Na ukazidi kunena: "Na si tuliona, pale Mlandege,
kulikuwa na akina mama watu wazima pia. Katika Tanzania hii, ukiona mikutano ya
Chama cha siasa inaanza kuhudhuriwa na akina mama watu wazima, basi, hicho si
chama cha kukibeza."
Hizi tafakuri zako tunduizi zimenigusa kwani ni
sawasawa na zangu tangu niliposhuhudia mkuatano wa kwanza wa kampeni ya kwanza
Dar es Saalaam ya kunadi Dr. Slaa kama ngombea wa Urais kwa tiketi ya Chadema
viwanja vya Jangwani mwaka jana.Nakushukuru sana Ndugu Mjengwa kwa kutumegea
busara yako kwa kuongozwa na imani ya TANU uliyonukuu ya "Nitasema kweli
daima, fitina kwangu mwiko". Asante Ndugu Mjengwa . Labda tembelea Njombe na
Songea upate kujua mikutano na maandamano ya Chadema huko yalikuwaje na
utujulishe kwa Kiswahili chako chenye lafudhi ya karafuu na alwa!!. Tusaidiane
kuendelea kuwasidia Watanzania wazidi kutambua ukweli unaozidi kupiga hodi
yeyote apende hasipende ambao ni kutaka kuongozwa na chama mbadala ya
CCM....
Wenzetu Zanzibar walau wamefanikiwa kulazimisha kuwepo serikali
yenye kuongozwa na CCM nusu na chama mbadala yake cha CUF nusu...Kujivua gamba
kwa ukweli ni kwa wana-CCM wenyewe kusaidiana na Watanzania wengine kuondoa
ukilitimba wa serikali ya Muungano kuongozwa na CCM pekee kulikodumu kwa miaka
50 sasa. Ndio maana mzee mmoja wa kijiji cha jirani na Chuo Kikuu cha Mzumbe
Mororgoro alitamka kwenye Kongamano la Katiba lililoandaliwa na Chuo Kikuu cha
Mzumbe Ijumaa iliyopita kuwa yeye ndiyo kwanza alikuawa ameiona Katiba ya sasa
ya Jamhuri ya Muungano lakini kwa vitendo vya serikali ya sasa basi Katiba hiyo
lazima haifai na ilikuwa muafaka ije mpya mbadala yake. Ndiyo maana unawanukuu
watu wakikwambia " Ah, CCM tumeichoka bwana!” Kwanini? Namwuliza jamaa wa
mtaani; ” Tumeichoka tu, basi!” Na kuna wanaosema mitaani; ” CCM ni Chama Cha
Mafisadi!”" Hayo ndiyo maoni ninayokumbana nayo mimi pia kila siku kote nchi
nzima nilikobahatika kupita hivi karibu: Dar es Salaam, Arusha, Kilimanjaro,
Morogoro, Mwanza, na Kagera. Asante sana Ndugu Mjengwa kwa maoni yako ya kina.
Elimu kweli haina mwisho.
Mwl. Lwaitama
Kwa Hisani ya www.mjengwa.blogspot.com
Loading...
Post a Comment
CodeNirvana