Loading...
Zitto: Waliozembea ajali meli Spice wawajibishwe
Sunday, 11 September 2011 20:52
MBUNGE wa Kigoma Kaskazini, kupitia tiketi ya Chadema, Zitto Kabwe, ametaka watu waliohusika na uzembe katika ajali ya meli Spice Islander, wawajibishwe mara moja.Meli hiyo ambayo hadi sasa haijafamika kuwa ilibeba kiasi gani na watu na mizigo, ilizama katika eneo la Nungwi katikati ya Unguja na Pemba mwishoni mwa wiki iliyopita.
Akizungumzia tukio hilo lililosababisha zaidi ya watu 180 kupoteza maisha na wengine zaidi ya 500 kuokolewa, Zitto alisema kulikuwa na uzembe mamlaka za usimamizi vya usafiri wa majini.Alisema kwa msingi huo, wahusika katika mamlaa hizo, wanapaswac kuwajibika.
"Tumeambiwa majeruhi na marehemu idadi yao sasa inafikia zaidi ya abiria 800. Juzi asubuhi (Jumamosi) tuliambiwa kwamba uwezo wa boti ya MV Spice Islander ilikuwa ni kubeba abiria 500 na wafanyakazi 12, hii inadhihirisha uzembe uliokuwapo,”alisema Zitto.
Alisema watu waliohusika na uzembe huo katika Serikali ya Mapinduziya Zanzibar, wanapaswa kuwajibika mara tu baada ya kumalizika kwa muda wa siku tatu za maambolezo.
Zitto aliwataja wanaopaswa kuwajibika kuwa ni pamoja na Mkuu wa Bandari ya Zanzibar, Mustafa Aboud Jumbe na Waziri wa Miundombinu Hamad Masoud. "Natambua, kufukuzwa kwao kazi hakutarudisha ndugu zetu duniani, lakini litakuwa somo kwa wengine kutorudia makosa kama hayo,” alisema Zitto.
Kuhusu TBC1
Mbunge huyo pia alikilalamikia Kituo cha Televisheni cha Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC1)kwa kushindwa kujulisha umma kwa uhakika, habari kuhusu tukio hilo wakati linatokea.
Alisema badala yake, kituo hicho kinachotumia fedha za walipakodi kujiendesha, kilikuwa kikionyesha vipindi vya burudani ikiwamo taarabu.
Zitto alisema ni dhahiri kwamba serikali inapaswa kuwachukulia hatua wahusika ili iwe fundisho katika siku za baadaye.Alisema TBCI ilipaswa kuipa uzito habari kuhusu ajali hiyo kwa kuwa ni chombo kinachoendeshwa kwa kodi za wananchi.
Habari
Kwa Hisani ya Mwananchi
Post a Comment
CodeNirvana