Loading...
Mh Godbless Lema amjibu Tendwa
Nawasalimu
Leo asubuhi nimesikia habari za uzushi na majungu kutoka katika gazeti la Chama Cha Mapinduzi Uhuru pamoja na gazeti la serikali la Habari leo .
Hivyo basi kilichosemwa na magezeti ya Uhuru na Habari leo ya leo tarehe 23/2/2012 ni uzushi na propaganda , Magazeti haya ya CCM yatatumika sana kipindi hiki kama yalivyotumika kule Igunga yalipojaribu kutaka kuwatenganisha watu hata kwa dini zao lakini baadae ukweli ulijulikana na ikawa aibu kwao .
Kwa zaidi ya miaka hamsini ya uhuru wa Taifa letu kutoka kwa mkoloni bado Watanzania wa Arumeru sio huru na Watanzania wote kwa ujumla bado wanaishi maisha magumu kama wakimbizi nje ya Nchi yao.
Ninafahamu wajibu wangu katika kupigania demokrasia safi ya Nchi yangu na wakati huu jimbo la Arumeru Mashariki litakuwa mfano wa mapambano hayo na nitakuwa mstari wa mbele bila hofu wala kumuogopa mtu yeyote na wa cheo chochote katika kupigania ukweli na haki.
Wajibu wangu na wa chama changu kwa sasa ni kutoa matumaini kwa watu wote wa Taifa letu , na tunazo sababu za msingi za kwenda kushinda jimbo la Arumeru na ni wito wangu kwa kila kijana wa Arumeru anayeishi mjini kuona fursa hii ni kwa ajili ya ukombozi wa Nchi yetu na sio Arumeru peke yake na hivyo kwenda kutoa elimu vijijini tulikoacha wazee wetu.
Jana nilikuwa Meru , wazee na vijana wamekataa kuburuzwa na siasa za CCM ambazo kwa miaka hamsini ya uhuru wa Nchi hii zimeshindwa kutatua matatizo yao bali kufikiri rushwa ya pesa kipindi hiki cha Kampeni ndio mahitaji yao ya Msingi.
Nimesikia Tendwa msajili wa vyama vya siasa naye ameanza kusaidia CCM kufanya propaganda chafu labda ni vyema akatambua wajibu wake na sio kuanza kufanya kazi za siasa za CCM ni vyema akajua kuwa yeyote anayeitetea uovu leo itakuwa hasara kwake au kwa familia yake kesho .
Mwisho .
Ninajua macho ya Watanzania yako Arumeru mashariki , Ninawatia moyo wale mlioko mbali lakini mnapenda mabadiliko , sisi tulioko huku tutapambana kwa niaba yenu kufa na kupona kuhakikisha haki, usawa, na demokrasia vinapata thamani halisi bila uhuni wowote kufanikiwa.
Msiogope pengine huwezi kabisa kufika Arumeru kusaidia ukombozi basi wewe huko uliko tuombee kwa Mwenyezi Mungu , hakika hatutakubali uhuni ,udhalimu , na Nguvu ya rushwa iwachagulie ndugu zetu wa Arumeru Mbunge , kama Mbunge mmoja wa CCM Mwigulu Nchemba alivyotamba jana pale katika Hotel ya Mount Meru kuwa pesa bado hazijaanza kumwagwa kwani ndio kwanza ziko njiani zinakuja.
Hata hivyo Msiogope Udhalimu utashidwa Arumeru ““ Ni Afadhali vita inayotafuta haki na usawa kuliko Amani inayopumbaza na kudhalilisha utu wa Mwanadamu .
Godbless J Lema (Mb)
Post a Comment
CodeNirvana