na Hellen Ngoromera
CHAMA cha Mapinduzi (CCM) kimetangaza ratiba ya uchukuaji na urejeshaji fomu wa kumpata mgombea wa kiti cha uwakilishi katika uchaguzi mdogo wa jimbo la Bububu unaotarajiwa kufanyika Septemba 16.
Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa, Itikadi na Uenezi wa CCCM, Nape Nnauye, alisema jana katika taarifa yake kwa vyombo vya habari kwamba hatua hiyo na nyingine ilifikiwa na Halmashauri Kuu ya Taifa katika kikao chake kilichoketi Mei 13 na 14 chini ya mwenyekiti wake, Dk. Jakaya Kikwete.
“…Pamoja na mambo mengine kilipitisha ratiba ya Chama cha Mapinduzi ya mchakato wa kumpata mgombea wa kiti cha uwakilishi katika uchaguzi mdogo wa jimbo la Bububu unaotarajiwa kufanyika Septemba,” alisema Nape.
Alisema ratiba ya chama kuhusu uchukuaji na urejeshwaji wa fomu za maombi ya uongozi wa CCM utafanyika Julai 26 hadi 29 mwaka huu wakati ratiba ya Tume ya Uchaguzi (ZEC) kuhusu uchaguzi wa Bububu inaonyesha kwamba zoezi la uchukuaji fomu na urejeshaji wa fomu za wagombea utafanyika kuanzia Agosti 22 hadi 30.
Alisema Julai 30 CCM itafanya mkutano mkuu wa jimbo la Bububu kupendekeza majina matatu ya watakaopitishwa kuwania nafasi hiyo na kwamba kampeni ya matawini zitaanza Julai 31 hadi Agosti 4.
Agosti 5 kutakuwa na kura za maoni matawini na kesho yake kutakuwa na kikao cha kamati ya siasa ya Wilaya ya Magharibi Unguja, Agosti 7 Kamati ya Siasa ya mkoa wa Mjini Magharibi Unguja itakaa na Agosti 9 Sekretarieti ya Kamati Maalumu ya Halmashauri Kuu ya Taifa.
Nape alisema kwamba Agosti 11 Kamati Maalumu ya Halmashauri Kuu ya Taifa itakutana, Agosti 13 kutakuwa na kikao cha Sektretarieti ya Halmashauri Kuu ya Taifa na Agosti 15 kutakuwa na Kamati Kuu ya CCM ambayo itafanya uteuzi wa mgombea.
Ratiba ya ZEC kuhusu uchaguzi huo wa Bububu inaonyesha kwamba kampeni za wagombea zitaanza rasmi Agosti 31 mwaka huu na kukoma Septemba 15 ili kuwapa fursa wananchi wa huko kumchagua Mwakilishi wanayemtaka Septemba 16 mwaka huu.
Katika hatua nyingine CCM, imetoa salamu za rambirambi kutokana na kifo cha muasisi wa TANU, Dk. Kyaruzi kilichotokea Mei 20, Bukoba mkoani Kagera.
Katibu wa CCM, Wilson Mukama, alisema kwamba chama chao kimepokea taarifa hizo kwa mshtuko na kwamba marehemu huyo atakumbukwa katika harakati zake za kupigania uhuru wa Tanganyika tangu akiwa mwanafunzi.
Na Tanzania Daima
Loading...
Post a Comment
CodeNirvana