Featured

    Featured Posts

    Social Icons

    .
Loading...

Komu apinga Mahakamani uchaguzi wabunge EALA




Mwandishi wetu
ALIYEKUWA mgombea ubunge wa Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA) kwa tiketi ya Chadema, Anthony Komu amefungua kesi Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma akitaka itengue matokeo ya ubunge kwa upande wa Tanzaniaya uchaguzi uliofanyika Aprili 17, mwaka huu.

“Ninapenda kuwafahamisha Watanzania wote wapenda haki kuwa nimefungua kesi Mahakama Kuu ya Tanzania Dodoma, kupinga uchaguzi wa Bunge la Afrika ya Mashariki uliofanyika Dodoma, Aprili 17, 2012. Kesi hiyo itatajwa kwa mara ya kwanza Mei 24, mwaka huu,” alisema Komu katika taarifa yake kwa vyombo vya habari.

Alisema amefanya uamuzi huo kwa kuwa: “Nimejiridhisha kwamba uongozi wa Bunge la Tanzania ulitengeneza utaratibu uliokinyima Chadema haki ya katika uchaguzi huo.”

Komu ambaye chama chake kilijitoa kabla ya upigaji kura kikipinga kile ilichokiita ukiukaji wa taratibu hizo, alifafanua kwamba: “Ninaamini kuwa Mahakama ni kisima cha haki; itapitia maombi yangu, itatoa haki pale panapostahili.”

Komu alisema chini ya Mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Kanuni za Uchaguzi wa Bunge la Afrika Mashariki, Kanuni za Bunge la Tanzania; toleo la 2007 na sheria ya uchaguzi ya Tanzania; haki kwa matakwa ya sheria hizo havikuzingatiwa.

“Uongozi wa Bunge ulipaswa kuhakikisha uchaguzi unafanywa kwa namna ambayo uwiano wa vyama kulingana na idadi ya wabunge walioko bungeni ungezingatiwa, alisema na kuongeza:
“Hii ni kinyume cha mkataba wa kuanzisha Jumuiya Afrika Mashariki, Kifungu 50(1) na Kifungu cha 12 cha Kanuni za Bunge la Tanzania.”

Alisema uongozi wa Bunge ulipaswa kutoa viti tisa vya Tanzania kwa vyama vya siasa, jinsia, pande mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na makundi mengine maalumu na kuongeza: “Hili nalo halikuzingatiwa.”

Komu alisema uongozi wa Bunge haukuweka wazi ni kanuni ipi ilitumika katika kugawa viti hivyo vya Tanzania kwa makundi mbalimbali, bali uliamua kwa makosa au kwa makusudi kutozingatia uamuzi wa watangulizi wao.

“Tarehe 17 Novemba, 2006, aliyekuwa Spika wa Bunge, Samuel Sitta alitoa uamuzi kuhusu mgawanyo wa viti hivyo uamuzi ambao ungezingatiwa kusingekuwa na malalamiko yoyote leo,” alisema.

Katika madai yake, Komu anataka matokeo ya uchaguzi huo yabatilishwe, uitwishwe uchaguzi mpya na ufanywe baada ya kanuni zitakazozingatia mkataba wa kuanzishwa kwa EAC, Kifungu cha 50 (1).

“Taarifa hii itakuwa ujumbe kwa Watanzania wapenda haki kuwa lengo ni kujenga mfumo ambao utahakikisha haki ya kila mmoja, kulingana na sheria na taratibu ambazo tumejiwekea, tofauti na sasa ambapo masuala mengi yanategemea zaidi mapenzi ya watu walio madarakani,” alisema na kuongeza:

“Mtu yeyote makini akifanya utafiti namna ambavyo uchaguzi wa Bunge la Afrika Mashariki ulivyoendeshwa katika mabunge ya nchi washirika wa EAC katika mabunge yao (tofauti na Tanzania), anaweza kuona wazi kuwa Chadema haikutendewa haki na uongozi wa Bunge letu, baada ya kuamua kujitungia utaratibu wake mwenyewe.”
Source:Mwananchi
author

This post was written by: Author Name

Your description comes here!

Get Free Email Updates to your Inbox!
© Copyright Udaku Kijiweni
Back To Top