Loading...
JINSI YA KUTUMIA TWITTER ILI KUKUZA/KUTANGAZA BIASHARA YAKO
Makampuni mengi siku hizi yanatumia mtandao jamii wa Twitter kwa minajili ya kutangaza biashara zao na hivyo kuongeza kiwango cha mauzo yao kwa kupata au kuvutia wateja wengi zaidi. Ukikuta kampuni au biashara haiutumii mtandao wa Twitter kwa kuwasiliana na wateja waliopo na wa mbeleni,basi tambua kwamba kampuni hiyo haiendi na wakati. Yaweza kuwa kwa makusudi au kwa kutokutambua tu faida zilizopo katika matumizi ya Twitter na hata mitandao mingine ya kijamii(Social Networks).
Pamoja na kuzidisha matumizi ya Twitter, yapo makampuni, makubwa kwa madogo, ambayo bado wanashangaa kwamba inakuwaje watu wanaowafuata(Followers) hawajaweza bado kubadilika na kuwa zaidi ya wafuatiliaji tu na badala yake kuwa wanunuzi wa bidhaa au huduma. Kwanini?
Ni wazi na ukweli kwamba Twitter ni sehemu nzuri ya kutangazia biashara, matukio, kampeni za kusaidiana(kuchangishana fedha na mambo kama hayo) achilia mbali sehemu nzuri ya kupashana habari,kuelimika na kuburudisha kama ambavyo niliwahi kuandika katika post hii hapa.
Lakini kuandika tu (Tweets) haitoshi kukusaidia kukuza biashara kwa maana ya kuongeza wateja na kipato. Unahitaji uelewa wa ndani zaidi juu ya hadhira yako(audience), uwe na mpango thabiti wa mitandao jamii na uwe na njia mahususi ya kupima mafanikio yako kupitia Twitter. Muhimu zaidi unahitaji kujua jinsi gani na kwa namna gani utatumia Twitter kabla hujaanza. Haya hapa ni mambo machache unayoweza kuzingatia;
Fanya Utafiti: Utafiti kuhusu soko lako(Market Research) ni kitu cha lazima endapo unataka kuongeza nafasi za mafanikio yako. Kuuliza maswali muhimu na yanayoeleweka kwa jamii ya Twitter ni njia nzuri na rahisi ya kuelewa kwa undani kuhusu yaliyo muhimu kwa wateja wako.Wanataka nini? Ni kitu gani wanakitazamia kutoka kwako au kwa biashara yako.Ni aina gani za huduma ambazo wanazipendelea zaidi kutoka katika biashara yako? Ni kitu au vitu gani vinavyochangia maamuzi yao ya kutumia au kuchagua huduma au bidhaa kutoka kwako? Wanasemaje au wana maoni gani kuhusu washindani wako wa biashara.
Ukitenga muda maalumu wa ku-tweet kwa minajili ya kupata undani wa soko, bila shaka wateja wako, wa sasa na hata wa baadae, watakuchukulia kama mtu ambaye unaingilika, unasikiliza na wanaweza wakajisikia huru zaidi kutumia huduma au bidhaa kutoka kwako.Unakuwa karibu zaidi nao na unawajali.
Kuwa na Mpango/Mbinu Maalumu: Biashara za aina zote, zinahitaji kuwa na mpango maalumu wa kuwapata wateja, kubakia nao na kujenga msingi imara wa wateja hao kitu ambacho ni muhimu sana kwa maendeleo ya kweli ya biashara. Pamoja na njia zote za matangazo bado neno la kuambiwa kutoka kinywani kwa mtu mwingine(word of mouth) lina maana zaidi.Huo ni msingi.
Kwa hiyo kabla ya kuanza ku-tweet, jaribu kwanza kufanya utafiti kuhusiana na jamii yako ya mtandaoni(online community) na jinsi gani ujiingize au ushiriki katika jamii hiyo ukiwa miongoni mwao. Weka mpango madhubuti wa jinsi utakavyokuwa ukituma au ku-post tweet zako, mara ngapi utakuwa unafanya hivyo bila kusahau kuzingatia utakachokuwa una-post.
Muhimu zaidi hapa ni kuzingatia je hiki ninacho-post kitaamsha hisia za mtu kubofya(kama umeweka link kwa mfano), na je hii Tweet yangu itaongeza uelewa kwa wateja wangu,wa sasa na wa baadae, juu ya aina au huduma tunazotoa? Je, tweet hii itapelekea kuongezeka kwa masoko? Kwa tweet hii,wateja zaidi watashawishika kutumia bidhaa au huduma zinazotolewa na biashara yangu? Hayo ni baadhi ya maswali muhimu ya kujiuliza
Hakikisha wateja wanaelewa undani wa Bidhaa/Huduma zako: Kabla biashara yako haijaanza kutengeneza pesa, inahitaji kujenga kitu kinachoitwa social media magnetism. Hii tunaweza kusema ni sumaku ya/ndani ya mitandao jamii. Cha kwanza kufanya hapa ni kutumia watu unaojuana nao au ambao wanajua kuhusu biashara yako(watu wako wa karibu na watu unaokutana nao ana kwa ana wanafaa sana hapa) kwa ajili ya kuitambulisha biashara yako na kuwashawishi wengine watue kwenye ukurasa wako wa Twitter na hivyo wafuate brand yako.
Hapa ndipo panapokuwa na umuhimu wa kutumia jina linakubalika au kutambulika kirahisi.Kuwa na logo na kuitumia hiyo logo katika kila kitu kinachohusiana na biashara yako.Hakikisha kwamba ukurasa wako wa Twitter,unatambulika hivyo kwanza.
Kisha wafuate(Follow) wataalamu au wazoefu wengine katika aina ya biashara unayofanya. Yafuate makampuni mengine, wafuate washindani wako wa kibiashara. Changia mawazo hususani kuhusu utaalamu ulionao ili kuongeza heshima yako katika sekta. Kwa kufanya hivyo pia utakuwa unaongeza imani miongoni mwa wateja wako.Watakukubali zaidi. Chagua aina mahususi ya kushiriki katika mijadala mbalimbali kuhusiana na sekta au aina yako ya biashara.Chagua “sauti” ambayo itakuwa ni rahisi kwa watu kutambua.Ninaposema sauti ninamaanisha aina ya ujibuji maswali au uchangiaji.
Shirikisha Wateja Wako: Miongoni mwa makosa makubwa ambayo wamiliki wa biashara wanayoyafanya ni kutokuwa karibu na wateja wao. Ninapoongelea kuwashirikisha wateja wako ninamaanisha kuwa karibu nao.Kuwasikiliza kwa makini juu ya malalamiko,matarajio yao nk. Mitandao jamii ni sehemu nzuri ya mazungumzo au mijadala. Kwa maana hiyo, usiache kuwajibu wateja wako hususani katika zile Tweets ambazo zinaitaja au kuhitaji majibu kutoka kwako. Anzisha mazungumzo na pia shiriki mazungumzo. Katika mazungumzo hayo kuwa mkweli,muaminifu na utoe habari au taarifa ambazo zimefanyiwa utafiti.Usikurupuke.
Wajali wafuasi wako: Kadiri wateja wanavyozidi kuwa wengi,(hususani kwa makampuni au biashara ndogo ndogo) uwepo wako mtandaoni unaweza kupungua kwa kisingizio cha kuwa “busy”.Usifanye hilo kosa. Hakikisha kwamba unaendelea kuwepo mtandaoni.Hakikisha kwamba unaendelea kufanya yote niliyoyataja hapo juu ikiwemo kushiriki mijadala, kuuliza maswali ili kupata undani wa soko, kushughulikia malalamiko nk. Biashara nyingi zimekuwa zikitumia Twitter kama chombo cha kuhakikisha kwamba wateja wanaendelea kutumia bidhaa au huduma zao.
Tumia pia fursa hii kuwajulisha wateja wako kuhusiana na kile kinachoendelea katika sehemu yako ya biashara. Kama utakuwa umefunga kwa sababu moja au nyingine, waambie.Kama una punguzo la bei kwa bidhaa au huduma,waambie. Washirikishe kwa kila namna.Kwa kufanya hivyo kwanza hawatokusahau na pia wataona ni jinsi gani unavyowajali. Kila la kheri katika biashara yako.
Jeff Msangi ni Mhariri Mkuu wa www.bongocelebrity.com. Unaweza kuwasiliana naye kupitia jeffmsangi at gmail.com au jeffmsangi at bongocelebrity.com
Read more: JINSI YA KUTUMIA TWITTER ILI KUKUZA/KUTANGAZA BIASHARA YAKO - BongoCelebrity
Post a Comment
CodeNirvana