Loading...
Millya akoleza moto wa Lowassa CCM
Fidelis Butahe
WAKATI kada wa CCM na Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa akisema tatizo la chama hicho ni uongozi, mshirika wake kisiasa, James Ole Millya ambaye amejiunga Chadema hivi karibuni amejitokeza na kumuunga mkono huku akisema tatizo jingine linalokikabili chama hicho tawala ni makundi.
Mbali ya Ole Millya, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Monduli, Ruben Olekuney naye ameibuka na kusema kwamba Katibu Mkuu wa CCM, Wilson Mukama amekurupuka kumjibu Lowassa.
Mwishoni mwa wiki akiwa katika mkutano wa hadhara huko Mto wa Mbu, Arusha, Lowassa alisema tatizo la CCM ni uongozi kuacha kusimamia misingi. Hata hivyo, kauli hiyo ilipingwa vikali na Mukama ambaye alimtaka mbunge huyo wa Monduli kushughulikia matatizo jimboni kwake kwanza.
Millya ambaye anafahamika kuwa kijana mshirika mkubwa wa kisiasa wa Lowassa, aliibuka na kuzidi kukilipua chama hicho akisema, makundi hayo yameanzia ngazi ya taifa mpaka kwa wenyeviti wa serikali za mitaa.
Ole Millya alijivua nyadhifa zake zote ndani ya chama hicho kuanzia ngazi ya taifa Aprili 15, mwaka huu na kujiunga na Chadema, huku akidai kuwa CCM kimefilisika kimawazo na hakitoi matumaini kwa Watanzania.
Juzi, akiongea kwa njia ya simu alisema kwamba CCM kimekosa uongozi madhubuti na hakifai kuongoza nchi kwa kuwa kila kiongozi ana kundi lake. “Chama kikishafikia hatua hiyo huhitaji tena kuwemo ndiyo maana niliamua kuhamia Chadema kwa sababu hata viongozi wakongwe wa CCM akiwamo Mkurugenzi wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku, kada mkongwe wa chama hicho, John Kaduma na aliyewahi kuwa waziri katika Serikali ya Awamu ya Tatu, Hassy Kitine wameshaeleza udhaifu wa CCM,” alisema Millya.
“Watanzania wanatakiwa kukichagua Chadema kwa kuwa ndicho mbadala kwa CCM…, wasidanganywe. Nchi kama Marekani, Ufaransa, Uingereza na hata Kenya mambo yamekuwa mazuri baada ya wapinzani kupewa ridhaa ya kuongoza nchi na wananchi,” alisema Millya.
Alisema uongozi mbovu ndani ya CCM unazaa uongozi mbaya wa Serikali kwa kuwa wao ndiyo wanaoiongoza. Mwenyekiti wa CCM Monduli Akizungumzia kauli ya Mukama, Olekuney alisema Lowassa alikuwa akizungumzia uongozi wa chama hicho eneo la Mto wa Mbu na si wilaya, mkoa au taifa.
“Katika ziara tuliyofanya na Mh Lowassa Mto wa Mbu, kero nyingi ziliibuka na kero hizo zilikwishapelekwa kwenye ngazi ya kata lakini, hazikushughulikiwa na wanachama wakatishia kukihama chama kwani kero zao hazijashughulikiwa,” alisema na kuongeza kuwa hali ilikuwa tete kwa upande wa CCM eneo hilo la Mto wa Mbu.
Aliongeza: “Unajua watu wanamwamini na kumpenda huyu mzee sasa tulipokwenda pale tukakubaliana kuchukua uamuzi wa haraka na kweli ikasaidia, ndipo katika mkutano ule Edward (Lowassa) akasema kuna tatizo la uongozi kwenye chama, lakini chama ni kizuri akimaanisha chama ngazi ya kata ile.”
Alisema ni kweli kulikuwa na udhaifu kwenye uongozi wa kata na wamechukua hatua kwa kumpa onyo diwani wa eneo hilo kwa kutoa vibali vya ardhi bila ya kufuata taratibu zilizopo.
“Kwa kweli Mzee Mukama anatakiwa kwanza asome ‘content’ (maudhui) ya yale aliyosema Edward siyo kukurupuka, huku kwenye ngazi ya chini kuna matatizo makubwa ya uongozi. Kwanza alitakiwa aje kusaidiana nasi kukabiliana na kasi ya Chadema na siyo kukurupuka,” alisisitiza.
Mwenyekiti huyo wa CCM Monduli alisisitiza kuwa mbunge huyo wa Monduli katika ziara yake hiyo amefanikiwa kwa kiasi kikubwa kutuliza kasi ya upepo wa wanaCCM kukimbilia upinzani.
“Hii kazi ilitakiwa ifanywe na kina Mzee Mukama, sasa Edward sielewi wanamshutumu kwa lipi wakati amekuja kuimarisha uhai wa chama. Si aulize kwanza kuliko kukurupuka tu magazetini?”
Alivyosema Lowassa Katika mkutano huo, Lowassa aliwaambia wananchi kuwa, CCM kinakabiliwa na matatizo ya kiutendaji na uongozi, lakini kuna mambo matano yanayomfanya aendelee kuwa mwanachama wake.
Aliyataja mambo hayo kuwa ni muundo mzuri wa chama, kutetea wanyonge, kudumisha umoja na mshikamano, kuwalinda raia wa kawaida katika kupata na kufaidi rasilimali za nchi dhidi ya matajiri na wawekezaji wa nje na mfumo mzuri unaowezesha watu kujisahihisha na kusema kuwa kitakapoacha misingi yake ya awali ikiwemo kutetea wanyonge, hatakuwa mmoja wa wanachama wake.
“Pamoja na uzuri wake, muundo wa chama chetu ni mzuri sana, imani ya chama chetu ni nzuri sana, misingi inayoongoza chama chetu ni mizuri sana, lakini tuna tatizo la utendaji na uongozi ndani ya chama chetu …ama katika kufanya uamuzi au uamuzi usio sahihi au kutochukua hatua kwa matatizo yanayowakabili wananchi kwa wakati mwafaka.
Tukionekana hatujali shida za wananchi wetu, watatafuta mbadala , lakini kero hizi zishughulikiwe kwenye vikao.” Hata hivyo, Mukama alimjibu siku moja baadaye akisema haikuwa sahihi kwa Lowassa kutoa kauli hiyo kwenye mikutano ya hadhara wakati anajua bayana taratibu za chama hicho.
Alisema alipaswa kuzungumzia matatizo ya jimbo lake yakiwemo migogoro ya ardhi, wawekezaji na wananchi, wakulima na wafugaji, maji na kero nyingine mbalimbali na si kukishambulia CCM.
Alisisitiza kuwa kama Lowassa amebaini matatizo ya uongozi ndani ya CCM, alipaswa kuyazungumzia ndani ya vikao vya chama kwa sababu ana mamlaka ya kukosoa au kurekebisha, lakini si kwenda kwenye mikutano hiyo na kuanza kutoa kasoro wakati bado yumo ndani ya chama na ameshika nyadhifa mbalimbali.
Na Mwananchi
Post a Comment
CodeNirvana