Featured

    Featured Posts

    Social Icons

    .
Loading...

Nassari ashikiliwa polisi kwa saa saba



Tuesday, 08 May 2012
Musa Juma na Peter Saramba, Arusha
POLISI mkoani Arusha jana lilimhoji Mbunge wa Arumeru Mashariki (Chadema), Joshua Nassari kwa zaidi ya saa saba baada ya kujisalimisha katika Kituo Kikuu cha jeshi hilo.

Nassari ambaye anadaiwa kutoa maneno ya uchochezi dhidi ya Serikali katika mkutano wa hadhara wa Chadema uliofanyika Mei 5, mwaka huu katika Uwanja cha NMC, alishikiliwa kituoni hapo kuanzia 6:12 mchana hadi saa 12 jioni kisha kuruhusiwa kuondoka na kutakiwa kuripoti kituoni hapo leo.

Alifika hapo akiwa na Wakili wake, Arbert Msando bila ya kuwakuta viongozi wa jeshi hilo hivyo wakaamua kuondoka.

Lakini nusu sasa baadaye, Naibu Kamishna, Isaya Mungulu na Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Akilimali Mpwapwa walifika na kuwataka viongozi wa Chadema, waliokuwa kituoni hapo kuwasiliana na Nassari ili arejee.

Mjumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho, Godbless Lema aliyekuwapo aliwasiliana na Nassari ambaye alirejea saa 7:20 akiwa na Wakili Msando na alichukuliwa na Kamanda Mpwapwa ambaye alimwelekeza kuelekea Ofisi ya Mkuu wa
Upelelezi Mkoa (RCO) kwa mahojiano.

Baada ya kumfikisha Mbunge huyo katika ofisi za mahojiano, Kamanda Mpwapwa alisema kulingana na uzito wa shauri lake atalazimika kutafuta watu wa kumwekea dhamana mara baada ya kuhojiwa.

“Hapa yupo mikononi mwa polisi, atahojiwa na baadaye atapewa dhamana,” alisema Mpwapwa.

Kamishna Msaidizi wa Polisi, Salum Msangi kutoka Makao Makuu ya Idaya ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (CID), ndiye alikuwa akiongoza kikosi maalumu kilichokuwa kikimhoji Nassari.

Msangi ambaye ameteuliwa hivi karibuni kuwa Kamanda wa Polisi Mkoa mpya wa Simiyu, alikuwa akisaidiana na Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP), Hamisi Warioba kutoka ofisi ya upelelezi Mkoa wa Arusha.

ASP Warioba ndiye aliyewahoji watuhumiwa wengine, John Heche na Ally Bananga juzi kwa zaidi ya saa tisa kuanzia saa 4:00 asubuhi hadi saa 2:00 usiku, walipoachiwa kwa dhamana na kutakiwa kurejea jana asubuhi.

Awali, Nassari alieleza alikuwa hana taarifa za kuitwa polisi kwa shtaka lolote bali, mara baada ya mkutano huo wa Mei 5, alipokea ujumbe wa simu kutoka Ofisa Upelelezi Mkoa wa Arusha, Faustine Mafwere kuwa Kamanda wa Polisi Mkoa Arusha, Thobias Andengenye alikuwa anamtafuta ili waagane baada ya kuhamishiwa makao makuu.

“Mimi nimeshangaa leo kusoma katika vyombo vya habari kuwa nasakwa na polisi na ndiyo sababu nimekuja kwani awali, nilijua rafiki yangu Andengenye anataka tuagane na nilipanga siku nyingine,” alisema Nassari.

Nassari pamoja na viongozi wengine wa Chadema wanatuhumiwa kutoa kauli mbalimbali za uchochezi ikiwamo, kutishia kujitangazia uhuru wa
Arusha na kanda ya ziwa kama polisi haitawakamata waliohusika na mauaji ya mwenyekiti wa chama hicho Kata ya Usa River, Msafiri Mbwambo.

Pia alimtuhumu mtoto wa Rais, Ridhiwan Kikwete kushinikiza uteuzi wa baadhi ya viongozi serikalini.

Bananga ambaye pamoja na Heche pia walikuwa wakisubiri kuhojiwa zaidi jana alisema juzi aliulizwa juu ya kauli zao kwenye mkutano huo, dhidi ya Rais Kikwete na mtoto wake Ridhiwan. Huku Heche akisema kwamba aliulizwa juu kauli za Nassari katika mkutano huo.

Na Mwananchi
author

This post was written by: Author Name

Your description comes here!

Get Free Email Updates to your Inbox!
© Copyright 2025 Udaku Kijiweni | Designed By Code Nirvana