Featured

    Featured Posts

    Social Icons

    .
Loading...

Ni mtandao wa ushindi 2015



Elias Msuya
BAADA ya kufanyika kwa mabadiliko katika Baraza la Mawaziri hivi karibuni, Rais Jakaya Kikwete amefanya mabadiliko ya wakuu wa wilaya zote nchini, huku akiwatupa nje 31 na kuteua wapya 70 kati ya 133 walioteuliwa.

Katika mabadiliko hayo, Rais Kikwete amewahamisha wakuu wa wilaya 48, wakati waliobaki katika vituo vyao vya awali ni 15 tu. Kabla ya kutangazwa, nafasi za wakuu wa wilaya 20 zilikuwa wazi kutokana na sababu mbalimbali, zikiwamo waliokuwa wakuu wake kuteuliwa kushika nafasi nyingine za uongozi ndani na nje ya Serikali.

Miongoni mwa wakuu wa wilaya wapya, wamo waandishi wa habari watano, wabunge wa viti maalumu na waliokuwa wabunge katika kipindi cha 2005 – 2010 ambao walipoteza nafasi zao katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 31, 2010.

Waziri Mkuu Mizengo Pinda ndiye aliyetangaza mabadiliko hayo ofisini kwake Dar es Salaam ambapo alisema awali kulikuwa na wilaya 114 lakini baada ya Rais Kikwete kuanzisha wilaya mpya 19, idadi ya wilaya zote nchini zimefikia 133 na kwamba uteuzi umezingatia idadi hiyo.

Kupangwa kwa safu hiyo kumeelezwa kuwa ni mikakati ya Chama Cha Mapinduzi kujijenga kimtandao kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.

Hali hiyo inatokana na ukweli kwamba Katiba ya CCM inawatambua wakuu wa wilaya kuwa wajumbe wa Kamati za Siasa za Wilaya, wakati wakuu wa mikoa ni wajumbe wa kamati za siasa za ngazi hizo.

Kwa kuwa wajumbe hao ni wateule wa Rais hutizamwa ndani ya chama hicho kama watu muhimu ambao hulinda maslahi ya mamlaka zilizowateua, hivyo misimamo yao katika vikao hivyo huwa na nguvu kubwa ya ushawishi wa kimaamuzi.

Wakuu wa wilaya na mkakati wa ushindi CCM 2015
Akitoa maoni yake kuhusu upangwaji wa nafasi hizo, Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba, Deus Kibamba anasema nafasi za wakuu wa wilaya hazitambuliki kikatiba na kwamba hayo ndiyo mambo ya kuyabadilisha katika mchakato wa Katiba mpya.

“Nafasi hizi za wakuu wa wilaya hazipo hata kwenye Katiba, sana sana imezungumzia majukumu tu ya wakuu wa mikoa. Sasa sijui iliwasahau au vipi,” anasema Kibamba na kuongeza;

“Hata Waziri Mkuu Mizengo Pinda aliyewatangaza hana mamlaka nao, kwa sababu wale wanaripoti kwa Rais. Yaani ni mbwembwe tu, ndiyo mwenyewe Pinda alisema kuwa ametumwa na Rais.”

Anaendelea kufafanua kwamba katika ngazi ya wilaya, majukumu yote yamewekwa kwa mkurugenzi hivyo hakuna tena sababu ya kuwa na wakuu wa wilaya.

“Katika ngazi ya wilaya, wakurugenzi wa wilaya ndiyo wenye majukumu yote, wale ndiyo wanaoshikilia Serikali za mitaa. Sasa mkuu wa wilaya anafanya nini tena?” anasema Kibamba.

Akitoa mfano, Kibamba anasema kutokana na mwingiliano wa majukumu wakuu wa wilaya wamekuwa wakijiingiza kwenye kazi zisizowahusu,

“Kulikuwa na DC katika wilaya ya Lushoto (anamtaja jina) ambaye aliingilia kazi ya kutatua migogoro ya ardhi wakati yeye hahusiki. Majukumu yote yako kwa Mkurugenzi. Zamani wale wataalamu wote wa halmashauri walikuwa chini ya DC, lakini siku hizi wamewekwa kwa mkurugenzi. Dc amebaki na katibu tawala (Das) na mwanasheria,” anasema.

Kibamba anasema japo huu utakuwa ni uteuzi mkubwa wa mwisho kwa Rais Kikwete, lakini atakuwa amevuruga mkakati wake wa kuisafissha serikali kwani ameongeza mzigo mzito wa matumizi huku nchi ikiwa masikini.

“Nadhani huu ni uteuzi wa mwisho, lakini hauna maana kwakuwa ni kuiingiza tu Serikali kwenye matumizi makubwa yasiyo na msingi. Hivi sasa Serikali inaingia gharama ya kununua mashangingi mapya 133 kwa wakuu wa wilaya tu. Hata wizara alizounda hivi karibuni ni yale yale, ni nyingi mno”.

Kwa upande mwingine Kibamba anasema kuwa huo ni mkakati wa chama tawala kujipanga na uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.

“Ni kweli kabisa, huu ni mkakati wa kujipanga na uchaguzi kwasababu alichofanya ni kuokoteza tu makada wa CCM na kupachika. Kibaya zaidi ameokoteza makada waliokataliwa na wananchi kwenye kura za maoni za CCM.

Yaani siku hizi ukigombea ubunge kupitia CCM ukashindwa, ndiyo uimeingia kwenye droo ya kuteuliwa kuwa mkuu wa wilaya,” anasema Kibamba.

Naye Mhadhiri wa Sayansi ya siasa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Bashiru Ally anaunga mkono hoja ya CCM kujipanga kwaajili ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.

“Chama chochote cha siasa hujipanga kwa uchaguzi na kama chama kiko madarakani kinapata ahueni (incumbency advantage). Kwa hiyo kinatumia uteuzi wa wakuu wa wilaya, wakuu wa mikoa, viongozi wa majeshi, hazina, wafanyabiashara, wakwepa kodi na kila takataka ili kukisaidia chama kishinde,” anasema Bashiru.

Kutokana na hali hiyo anasema kazi ya kuwatumikia wananchi kwa vyama vya siasa vya sasa haipo tena badala yake vyama vimekuwa kama mitambo ya kura tu.

“Kazi ya kuwatumikia wananchi ilifanywa na vyama vya ukombozi wakati ule, siku hizi hakuna tena. CCM sasa ni mtambo wa kura tu. Kikimaliza uchaguzi huu kinatayarisha uchaguzi mwingine, siyo kuwatumikia wananchi tena” anasema na kuongeza,

“Siyo CCM tu, hata ANC ile ya Mandela haipo tena, usione kina Julius Malema wakilumbana pale, wanatafuta ulaji tu.”

Bashiru anasema kama kuna ulazima wa kuendelea kuwa na nafasi za wakuu wa wilaya, basi wapigiwe kura kwani hakuna sifa maalumu ya kupewa nafasi hiyo.

“Kwa hali iliyopo sasa ni vigumu kujua mkuu wa wilaya anafanya kazi gani. Kwa mfano jiulize, kabla ya uteuzi huu, wilaya za Ilala na Temeke hazikuwa na wakuu wa wilaya, badala yake akawa ana kaimu mkuu wa wilaya ya Kinondoni Jordan Rugimbana na mambo yalikwenda vizuri tu. Sasa kama mwaka mzima unapita bila wakuu wa wilaya kubwa kama hizo nchini na mambo yakaenda kama kawaida, kuna haja gani ya kuwa nao?” anahoji Bashiru na kuongeza,

“Kama kuna haja ya kuendelea nao, basi wapigiwe kura ili tujue sifa zinazotumika kuwapata. Maana haieleweki, utakuta mwingine ana shahada ya uzamivu, mwingine ni mkulima tu, mwingine ni mstaafu wa jeshi, mwingine ameshindwa uchaguzi, mwingine alikuwa naibu waziri sasa amekuwa DC, wapi na wapi? Watuambie ni sifa gani inampa mtu ukuu wa wilaya,” anasema Bashiru.

Akitoa maoni ya Chadema kuhusu uteuzi huo wa wakuu wa wilaya, Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa Chadema, John Mnyika anasema kundi hilo la wateule wa Rais ni mzigo kwa nchi kwa sababu hawana kazi ya kufanya zaidi ya kuwajibika kisiasa.

“Tunahitaji nini kutoka kwa Mkuu wa Wilaya, katika kila wilaya kuna madiwani wanaouchaguliwa na wananchi, wabunge na Meya ama mwenyekiti wa Halmashauri husika, kweli tunahitaji DC hapo?” anahoji na kuongeza,
“Pia kuna wakurugenzi wanaofanya kazi kwa niaba ya Serikali pamoja na watendaji wengine sasa hawa wakuu wa wilaya kazi zao zipi.”

“Chadema hatuwezi kupongeza uteuzi huo kwani hatutambui uwepo wao. Kimsingi, kundi hilo la wateule wa Rais halina kazi ya kufanya zaidi ya ile ya ujumbe katika Kamati za Siasa za Wilaya za CCM.”

Hata hivyo, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye anasema kuwa; kwa wale wasioridhishwa na uwapo wa wakuu wa wilaya wafikishe hoja zao kwenye Tume ya Marekebisho ya Katiba ili maoni yao yafanyiwe kazi.

Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Julius Mtatiro anasema chama chao hakioni umuhimu wa wakuu wa wilaya na kwamba hawana msaada wowote kwa wananchi bali wanalinda maslahi ya chama.

"Wakuu wa wilaya ni makada tu wa chama hivyo ni muhimu wachaguliwe na si kuteuliwa tu na Rais kwa kuwa wanajipa mamlaka makubwa," anasema Mtatiro.

Anasema nchi haihitaji makada wa CCM ambao wameshindwa kwenye ubunge na kushindwa kazi maeneo mengine wawekwe kwenye nafasi muhimu kama hizo.

"Wanakwenda kulinda maslahi ya CCM na si kuwasaidia wananchi. Ni bora hizi nafasi zifutwe au ziwekewe utaratibu wa kupatikana,"anasema Mtatiro.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu Dar es Salaam, Dk Benson Bana anasema uteuzi huo umelenga kuiimarisha CCM kutokana na vijana kupewa nafasi zaidi.

Amesema hizo ni dalili kwamba CCM kimeona nguvu ya upinzani na sasa kimeanza kujiimarisha kwa kuwatumia vijana na wakuu hao wa wilaya.

“Wamehofia kuwa wanaweza kwenda Chadema ndio maana wameamua kuwapa nafasi vijana, hiyo ni changamoto ambayo wameifanyia kazi,” anasema Dk Bana.

Kutoka Mwananchi online.
author

This post was written by: Author Name

Your description comes here!

Get Free Email Updates to your Inbox!
© Copyright Udaku Kijiweni
Back To Top