VUA GAMBA CHANA GWANDA VAA UZALENDO: Kwa kauli mbiu hii, CCM waipigia debe CHADEMA
Nimekuwa nikitafakari sana maana ya kauli mbiu za CCM na CHADEMA, katika kutafakari kwangu niligundua kuwa kumbe kauli zote mbili zinamaana moja au zinalenga dhana moja japo zipo katika mpangilio na idadi ya maneno tofauti. Hivi ndivyo tafakari yangu juu ya hizi kauli mbiu ilivyokuwa. Nianze na kaulimbiu moja moja.
CHADEMA wanasema:
“Vua gamba vaa gwanda”
Kwa wana CHADEMA neno ‘gamba’ humaanisha tabia mbaya za kifisadi ambazo watu/wanasiasa walio katika Chama tawala (CCM) wanazo, na kwamba mtu yeyote aliye mwanachama wa chama hicho ni gamba (fisadi) kwa namna moja au nyingine japo viwango vya ugamba vinatofautiana kulingana na umbali au ukaribu wa mwanachama na jikoni. Kwamba wengine ni magamba kwa sababu ya ujinga wao na si kwa utashi wao. Kwamba mtu yeyote ambaye ni mwanachama wa CCM ni gamba kwa sababu hiyo ya uanachama wake, kwasababu CCM katika uyenyewe au ulivyo wake kwa sasa ni GAMBA, kwa hiyo yeyote anayekishabikia ni gamba kwa sababu hiyo ama kwa kujua au kwa kutokujua.
Kitenzi ‘vua’ kinatumiwa badala ya maneno ‘kwangua’ au ‘chuna’ maana haya ndiyo maneno sahihi kutumiwa katika muktadha huu yakiwa yana maana ya ‘kuacha’. Gamba huwa limegandamana katika mwili wa kiumbe, hivyo ili kulitoa huwa linakwanguliwa na visu au mapanga makali. Kumbuka jinsi samaki wenye magamba ambavyo huwa wanakwanguliwa magamba na mkwanguaji anayaacha na kuchukua samaki aliyekwanguliwa tayari. Hivyo wana CHADEMA wanaposema Vua gamba… wanakuwa wanawataka hao walioelezewa hapo juu “kukwangua magamba…”
Neno “gwanda” kwa wana CHADEMA ni lugha ya picha, haliishii kwenye kumaanisha nguo kama nguo (in a literal sense of the word) katika u-nguo wake, la sivyo lingekuwa halina maana yoyote. Gwanda ni picha ya uzalendo, ni picha ya wapiganaji wazalendo wanaopigania wananchi kupata haki zao. Kwa hiyo mtu yeyote akikutana na mtu amevaa gwanda, jambo la kwanza litakalomwijia akilini ni kuwa huyu mtu ni mpiganaji mzalendo. Ndiyo wako waigizaji lakini mantiki ya msingi ya alama au picha hii ni ‘UZALENDO’
Kwa maana hizo hapo juu kauli mbiu ya CHADEMA yaweza kutamkwa tena hivi:“Acha (vua) ufisadi (gamba), kuwa (vaa) mzalendo (gwanda)” yaani “ Acha ufisadi, kuwa mzalendo”
CCM wanasema:
“Vua gamba, chana gwanda, vaa uzalendo”
Kumbe CCM na watu wake, wanakiri kuwa, kuna ufisadi (u-ganda) ndani yao, kwa hiyo wanaposema , “vua gamba…” wanakuwa na maana ile ile waliyonayo CHADEMA, na kwakweli ushuhuda wa mtu mwenyewe huwa na nguvu kuliko kusimuliwa na mtu mwingine kwasababu yeye ndiye anayekuwa anajijua undani wake.
“…chana gwanda…” msemo huu unamaana kubwa, kwamba si uvue tu bali uende mbali zaidi uchane gwanda lililokuwa linafunika gamba lisionekane machoni, yaani lililokuwa linawastili mbele za watu. Je, gwanda hili la wana CCM ni lipi? Je, ni lile la CHADEMA? Haliwezi kuwa kwa sababu ya maana halisi ya “gwanda” katika maana ya CHADEMA.
Tukijaribu kupima kama ndilo wanalomaanisha kwa kuchukua maana ya CHADEMA yaani ‘UZALENDO’ na kuliweka katika hiyo sentensi yao utaona mkanganyiko mkubwa. Mfano: Vua gamba, chana gwanda, vaa uzalendo” hii ndio kauli yao, sasa tuijaribu na maana ya CHADEMA: “ Vua gamba, chana uzalendo, vaa uzalendo” haina maana ni kujichanganya! Kumbe sasa wana maana nyingine ya kwao lakini yenye maana kubwa ya neno “gwanda” kwa hiyo haya ni magwanda mawili tofauti yenye maana mbili tofauti japo yametumia maneno fanano but referring to different concepts.
Maana ya neno gwanda kwa mtazamo wa CCM twaweza kuipata kwa kuangalia kitenzi kilicholitangulia “chana gwanda” CCM imetumia neno hili in a negative sense ikionesha mtazamo wao walionao kwa hili gwanda, kwamba linastahili kuchanwa kutokana na kuwa halina maana tena, ni chafu haliifai kuvaliwa. Jambo moja tu linalifaa- kuchanwa. Na mtu akichana nguo aliyokuwa anaivaa kwa sababu imejaa chawa na viroboto ni chafu inanuka, maana yake amepata nyingine ya kumstiri ambayo ni mpya! Litakuwa jambo la kushangaza na pengine utaitwa kichaa ukikutwa unachana nguo mpya! Hapa neno “GWANDA” humaanisha “CCM” gwanda fisadi au gwandagamba.
Ndio kusema kuwa CCM katika u-CCM wao wenyewe wanakiri kuwa si gwanda la kuvaliwa tena bali la kuchanwa. Kauli mbiu yao haiwaachi watu solemba bila kuonesha suluhisho, inashauri, “…vaa uzalendo”Ikimaanisha kwamba, “vaa gwanda” katika maana ya CHADEMA. Kwa mantiki hiyo CCM inawashauri wanachama wake KUICHANILIA MBALI CCM na kuvaa gwanda la CHADEMA.
Hii ndiyo tafakari yangu kwa leo wakuu wana JF wenzangu.
FUATILIA Mjadala huu:Jamii Forums.
Loading...
Post a Comment
CodeNirvana