
CHADEMA WAELEWA SASA MADHARA YA OIL CHAFU
CHAMA Cha Demokrasia na Maendeleo
(CHADEMA), kimetangaza rasmi kusitisha
kuwapokea viongozi wa ngazi zote
watakaohama kutoka Chama Cha Mapinduzi
(CCM) na vyama vingine, baada ya kutemwa
katika kura za maoni kwa lengo la kutaka
kuwania nafasi za uongozi ndani ya chama
hicho.
Mwenyekiti wa Taifa wa CHADEMA, Freeman
Mbowe, alitoa msimamo huo jana alipokutana
na wanafunzi wa vyuo vikuu vitatu vya Udom,
CBE na St John, katika hafla ya kuwaaga wenzao
wanaomaliza masomo yao.
Mbowe alisema kuwa, CHADEMA kinataka sasa
kupata viongozi na wanachama wanaosukumwa
na uzalendo wa kweli, na wanaoamini itikadi na
sera zake, na si wanaotaka kukitumia kama
ngazi ya kufanikisha malengo yao.
Alisema wamejifunza kwa kiasi kikubwa hasara
ya kuwapokea wanachama, na hasa waliokuwa
viongozi wa vyama vingine dakika za mwisho,
hususan wakati wa uchaguzi, hivyo kuanzia sasa
hawapo tayari kufanya hivyo.
Mbowe alisema wapo tayari na
wanawakaribisha wanachama ama viongozi wa
CCM ambao wanaona kuwa CHADEMA ni chama
makini, kikomavu na wanaoamini kina malengo
halisi ya kuikomboa nchi na kuwaletea
maendeleo wananchi wote bila kujali itikadi ya
vyama, dini, kabila ama eneo la nchi.
“Wale wapambanaji waliochoshwa na matendo
ya wenzao ndani ya CCM, na wanaoamini kwa
dhati kabisa na kusukumwa na dhamiri ya kweli
ya kupigania maslahi ya wanyonge, waje sasa.
“Hakuna haja ya wao kusubiri hadi dakika za
mwisho, na hasa pale wanapopigwa chini katika
kura za maoni ndio waje. Wajue kuwa
wakisubiri muda huo, hawataweza kupokelewa
hata kama watakuwa ni wazuri namna gani,”
alisema Mbowe.