Featured

    Featured Posts

    Social Icons

    .
Loading...

Ni vita ya NHC na wapangaji Upanga

SHIRIKA la Nyumba la Taifa (NHC) limethibitisha kwa vitendo kwamba nyumba zilizopo eneo la Upanga jijini hazitauzwa baada ya kuvunja jengo lake la makao makuu katika Mkoa wa Ilala na kutangaza kujenga makazi ya familia 200 katika eneo hilo.

Mkuu wa kitengo wa mahusiano NHC, Susan Omari alisema jana ofisi hiyo ambayo ipo kiwanja namba 290 Upanga Mtaa wa Magole na Vijibweni itahamia jengo la Matsalamat ghorofa ya kwanza, Mtaa wa Samora kiwanja namba 568/48 na kuanza kazi rasmi Julai mosi mwaka huu.

Aliwataka wateja wa NHC Upanga kulipia kodi zao katika ofisi za shirika hilo mtaa wa Nkurumah.

Hatua ya kuvunjwa kwa jengo hilo, imekuja wakati kukiwa na mvutano mkali baina ya NHC na wapangaji wa eneo hilo la Upanga ambao wamekuwa wakishinikiza wauziwe nyumba hizo kwa madai kwamba wameishi humo kwa muda mrefu.

Kufuatia mgogoro huo, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka leo anakutana na wapangaji hao pamoja Menejimenti ya NHC katika ukumbi wa Karimjee jijini Dar es Salaam ili kujaribu kufikia mwafaka wa suala hilo.

"Nimewaita hapa kwa sababu moja kubwa, NHC inahamisha ofisi zake za Upanga kwenda jengo la Matsalamat Mtaa wa Samora kuanzia Julai mosi mwaka huu kwa dhumuni la kuongeza makazi ya wananchi katika eneo hili," alisema Susan katika mkutano na wanahabari katika ofisi hizo.

Alisema ujenzi wa jengo hilo ambao unatarajiwa kuanza mwanzoni mwa mwaka ujao wa 2012 upo katika hatua za michoro ukilenga kuboresha matumizi ya ardhi na kuboresha makazi ya watu na mbali na makazi ya watu jengo hilo litakuwa na viwanja vya kuchezea watoto, maegesho ya magari na maduka.

Kwa mujibu wa Susan, sanjari na mradi huo NHC tayari imetangaza zabuni za kuendeleza maeneo ya Ngano na Msasani Mjini Dar es Salaam.Kuhusu wakazi wa zaidi ya 4,000 wa Upanga wanaokutana na Waziri wa Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka wakitaka kuuziwa nyumba za NHC, Susan alisema: “Kama shirika hatuuzi eneo la Upanga.

“Mkakati wa NHC ni kujenga maghorofa katika eneo hilo, ili yachukue watu wengi zaidi wa kipato cha chini, kipato cha kati na cha juu,"alisema.

Alisema lengo la shirika hilo ni kuboresha matumizi ya ardhi na kuwanufaisha wananchi wengi zaidi badala ya wachache na kwamba mpango wa NHC ni kuwauzia wananchi asilimia 70 ya nyumba itakazojengwa na asilimia 30 itakuwa kwa ajili ya kuwapangisha wananchi wasio na uwezo wa kununua nyumba hizo.

Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Nehemia Mchechu aliliambia Mwananchi kuwa mpango wa shirika lake ni kujenga nyumba zenye uwezo wa kuhifadhi familia 200,000 katika eneo hilo la Upanga, tofauti na sasa familia zisizozidi 4,000 zinaishi katika nyumba zilizopo katika eneo hilo.

“Maombi ya wapangaji hawa si tu kwamba yanapingana na sera ya makazi, lakini pia yanakiuka sheria ya manunuzi ya umma kwamba huwezi kuuza nyumba za serikali hivihivi, lazima zitangazwe na ziuzwe kwa tenda,”alisema Mchechu.Kauli hiyo ya NHC imekuja huku wapangaji hao wengi wakiwa na asili ya kiasia wakitaka kuuziwa nyumba za NHC walizopanga.

Juni 18 mwaka 2010 wapangaji hao walimwandikia mwenyekiti wa Bodi ya NHC maoni na mapendekezo kuhusu kodi na kuuziwa nyumba hizo.Katika moja ya vifungu vya barua hiyo wapangaji hao walisema:”Utangulizi huo muhimu kutoka mioyoni mwa wapangaji na wapiga kura wenu, hata kama kwa asilimia yao ni ndogo (lakini siyo ndogo kuliko waliouziwa nyumba za serikali na viwanja vyake vikubwa, tena kwa bei poa)."

“Kwa mujibu wa sheria mbili na kanuni zake zilizoanza kutumika Mei mosi mwaka 2009, wapangaji wanataka na wanaomba mchakato na utaratibu wa kumilikishwa sehemu za nyumba za ghorofa, uanze kwa kuzingatia na kufuata ipasavyo sheria mbili zilizopitishwa na Bunge bila kungoja mpaka NHC watakapokuwa tayari,"ilisema sehemu ya barua.

Wapangaji hao walipendekeza utaratibu huo ufanyike bila mtu yoyote kubaguliwa kwa misingi ya maeneo, hali, rangi na asili na pia walipendekeza kodi walizolipa kwa nyumba hizo zihesabiwe katika mchakato huo.

Tayari Waziri wa Nyumba na Maendeleo ya Makazi amekubali kukutana na wapoangaji hao pamoja na NHC na leo atafanya kikao katika ukumbi wa Karimjee jijini Dar es Salaam.

Chanzo:Mwananchi,
Exuper Kachenje
author

This post was written by: Author Name

Your description comes here!

Get Free Email Updates to your Inbox!
© Copyright Udaku Kijiweni
Back To Top