Featured

    Featured Posts

    Social Icons

    .
Loading...

Dk Kitila Mkumbo: Vijana wa BAVICHA wanahitaji kufundwa !

Malumbano baina ya Mwenyekiti wa BAVICHA na Makamu wake katika vyombo vya habari ni hatua ya kubalehe kisiasa, ambayo haipaswi kuwakatisha tamaa wapenzi wa mageuzi nchini. Bahati mbaya kubalehe huku kunaambatana na usumbufu na kero. Usumbufu na kero hizi zingekuwa za maana kama vijana hawa wangekuwa wanalumbana juu ya jambo la msingi la kifalsafa au kisera au kikanuni ndani ya chama na nchi. Bahati mbaya kwamba vijana hawa wanalumbana kwa jambo la kipuuzi. Ni upuuzi kulumbana juu ya kauli rejareja za Mbunge wa Maswa John Shibuda, mwanasiasa ambaye mbwembwe zake za kisiasa zinajulikana hata kabla hajahamia CHADEMA.

Kwamba Shibuda ametangaza kugombea urais ndani ya kikao cha CCM haiwezi kuwa tatizo kwa sababu kimsingi kufanya hivyo hakuvunji kanuni yeyote ndani ya CHADEMA kwa sababu hakuna kanuni yeyote inayoelekeza muda na mahali mwafaka pa kutangaza nia ya kugombea urais. Mwanachama anapaswa kuongozwa na busara zake tu juu ya muda na mahali pa kutangaza nia yake. Sasa kama mwanachama wa CHADEMA hana busara kiasi cha kutangaza nia ya kugombea urais ndani ya kikao cha ‘mpinzani’ wake CCM, na kama busara za mwanachama huyo ni finyu kiasi cha kumuomba mwenyekiti wa CCM ndiye awe meneja wa kampeni zake, kwa nini iwe tatizo kwa BAVICHA au CHADEMA?

Hivyo, haikutarajiwa kwamba kuna mtu mwenye akili sawasawa ndani ya CHADEMA angemjibu Shibuda pale alipotamka, ndani ya kikao cha CCM, kwamba angegombea urais kupitia CHADEMA mwaka 2015. Kauli ya Shibuda haikustahili kupewa umakini wowote hasa kwa kitendo chake cha kusema kwamba Rais Kikwete ndiye angekuwa meneja wake wa Kampeni. Hili peke yake lilitosha kuonyesha kwamba kauli za Shibuda ni mwendelezo wa mbwembwe zake kisiasa zisizostahili kupewa uzito wowote ule. Hivyo, kwa Mwenyekiti wa BAVICHA kutoa tamko kali juu ya Shibuda ilikuwa sawa na mtu mwenye akili timamu kujaribu kumkimbiza kichaa aliyekimbia na nguo zake. Ni vizuri wanasiasa vijana wakaielewa kwa upana wake dhana ya uhuru wa maoni. Uhuru wa maoni ni pamoja na kukubali kusikia yale usiyoyapenda na kuyataka.

Katika kujitutumua kisiasa, Makamu wa BAVICHA naye anatoa tamko la kumkana ‘bosi’ wake, tena hadharani na nje ya viwanja vya chama. Madai ya makamu huyu wa BAVICHA ni kwamba hakuna kikao kilichoidhinisha tamko la Mwenyekiti wa BAVICHA kusema hayo aliyoyasema. Haya, na yeye tunamuuliza kikao gani cha BAVICHA kiliidhinisha yeye kumpinga mwenyekiti wake hadharani mbele ya waandishi wa habari? Je, makamu wa BAVICHA aliona ugumu gani kwenda kumshtaki mwenyekiti wake kwenye vikao vya BAVICHA na/au CHADEMA?

Nafikiri vijana hawa wa BAVICHA wanahitaji kufundwa. Nawashauri viongozi wa CHADEMA kuchukua hatua muhimu za kuwafunda vijana wa BAVICHA ili ubalehe wao wa kisiasa upite bila madhara kwa chama. Kufundwa huko ni pamoja na kuwafundisha namna ya kufanya kazi na vyombo vya habari. Wanahitaji kuhariri matamko yao sawasawa, na kabla ya kuyatoa wapime athari za matamko yao kwa chama. Ukiona wewe ni kiongozi wa CHADEMA unatoa tamko na tamko hilo linapamba vichwa vya habari vya magazeti pinzani kwa chama chako kama vile Uhuru, ujue tamko lako limekiumiza chama.

Laiti viongozi wa BAVICHA wangekuwa makini wangejizuia kutoa matamko yao. Mwenyekiti wa BAVICHA angekuwa makini angetafakari maana ya kauli yake kabla hajaitoa, na angedundua kwamba tafsiri pana ya kauli yake ni kutaka kuzuia baadhi ya wanachama wa CHADEMA kugombea urais. Naye makamu wake angekuwa makini angetambua kwamba kumpinga mwenyekiti wake hadharani ni kutangaza mgogoro ndani ya chama, na ilikuwa ni kucheza mikononi mwa wapinzani wa CHADEMA. Viongozi hawa wanapaswa kutambua kwamba katika mawasiliano muhimu siyo unachosema, bali kile ambacho hadhira inasikia. Kwenye tamko la Mwenyekiti wa BAVICHA hadhira walisikia kwamba baadhi ya wanachama wa CHADEMA hawaruhusiwi kutangaza kugombea urais, na walichosikia hadhira ya makamu wake ni kwamba kuna mgogoro ndani ya CHADEMA! Je, huu ndio ujumbe ambao viongozi hawa walitarajia kuufikisha?

Msimamo wa CHADEMA dhidi ya kauli za Shibuda umekuwa ni ‘kumdharau’ kwani, pamoja na kwamba zinasababisha usumbufu, kauli zake zimekuwa hazina madhara ya msingi kisiasa kwa chama. Hata hivyo kauli za Shibuda iliyoripotiwa katika moja ya magazeti ya Jumapili ni zaidi ya usumbufu. Kwamba viongozi wa CHADEMA wanamchukia Shibuda kwa sababu ni msukuma ni kukigombanisha chama na wapiga kura wa kanda ya ziwa. Huu sasa sio usumbufu tena bali ni uharibifu. Usumbufu unavumilika, lakini uharibifu hauwezi kuvumilika. Ni wazi kuwa Shibuda amepania kuiharibu CHADEMA. Kwa hivyo kuna haja ya kuangalia upya sera ya kumdharau Shibuda.

Tukumbuke kwamba mambo yote haya yanatokea kipindi ambacho Waziri mwandamizi katika serikali ya CCM ameapa kuona CHADEMA inasambaratika ndani ya mwaka mmoja. Vijana wa BAVICHA yawapasa kuwa makini, vinginevyo wataonekana wapo katika mkakati wa kuisambaratisha CHADEMA. Tumewaonya!


Dk Kitila Mkumbo ni Mhadhiri Mwandamizi, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
Gazeti la Rai Mwema | Jumatano, 24 Mei 2012
author

This post was written by: Author Name

Your description comes here!

Get Free Email Updates to your Inbox!
© Copyright Udaku Kijiweni
Back To Top