Loading...
Hotuba ya mbowe mazishi ya Makani imebeba uzito stahiki unaofikirisha
Mbowe apasua jipu kwenye mazishi ya Makani
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, amewaonya wanasiasa wanaopenda kutumia propaganda chafu za udini kwa manufaa ya muda mfupi ya kisiasa ya vyama vyao kwa gharama ya kuwagawanya Watanzania na kulibomoa taifa lao.
Amesema kuwa amekuwa akishangazwa na unyenyekevu, ukaribu na ushirikiano unaooneshwa baina ya wanasiasa na viongozi mbalimbali wa kiserikali wakati wa misiba, lakini huonekana kusahahu kila kitu mara baada ya misiba na kuendekeza propaganda za udini na ukabila, badala ya kuweka mbele utaifa.
Akizungumza wakati wa kutoa salaam za rambimrambi kwa niaba ya Chadema mara baada ya mazishi ya mmoja wa wanasiasa wa chama hicho, Bob Mkani Makani, jana katika kijijini Ukenyenge, wilayani Kishapu, Mbowe alisema marehemu alikuwa mtu mzuri aliyejitoa kwa hali na mali kwa ajili ya Watanzania.
“Kwa ujumla niseme tu kuwa siwezi kutumia dakika tano hizi kumaliza kuzungumzia sifa za Bob, lakini niseme kuwa nimekuwa nashangazwa na unyenyekevu huu unaooneshwa wakati wa misiba pekee, wakati wa misiba kunakuwa na ukaribu na ushirikiano wa hali ya juu, lakini tunakuwa wepesi sana tunasahau punde tu…baada ya msiba tunarudi kunyukana tena kwa kutumia na kutanguliza propaganda mbalimbali zikiwemo za udini,” alisema na kuongeza:
“Mathalani leo wengine hapa walijua Bob ni Mkristo, kumbe Bob ni Mwislamu, lakini tumekuwa tunatumia propaganda nyepesi za udini tunaharibu historia makusudi kwa maslahi yetu mafupi ya kisiasa bila kujua kuwa wakati huo huo tunalibomoa taifa letu katika misingi ya udini.”
“Leo tumekaa wote hapa, watu wa dini mbalimbali, tuna viongozi wetu hapa wa dini mbalimbali, tumekaa pamoja kabisa tumevumiliana, wapo watu wa makabila mbalimbali…hakuna tatizo lolote kabisa, kwa sababu sisi hatupaswi kutambulishwa kwa makabila wala dini zetu bali tunatambulishwa kwa utaifa na Utanzania wetu basi,” aliongeza.
“Napenda kutoa hii rai leo kwa viongozi wa dini zote walioko mahali hapa, kwa viongozi wote wa vyama vya siasa na kwa viongozi wa serikali, vyama hivi vya siasa ni vitu vya kupita, tusibomoe utaifa wetu kwa bendera za vyama vyetu. Vyama vyote hivi Chadema na CCM vitapita, lakini Watanzania na nchi yao watabaki,” alisema Mbowe huku waombolezaji wakishindwa kujizuia kumpigia makofi mengi.
Mbowe alisema kuwa Hayati Bob alijitoa kwa hali na mali kwa ajili ya Watanzania akitolea mfano namna alivyojitolea nyumba yake maeneo ya Sea View, Dar es Salaam kuwa mahali pa vikao vya mwanzo kabisa kuanzisha chama hicho cha siasa.
“Wakati watu wengi wakiogopa kujihusisha na vyama vya upinzani Bob hakujali, kwa sababu Bob was a guy of courage (mtu jasiri). Hakuogopa. Akadiriki kuruhusu nyumbani kwake kuwa mahali pa vikao. Mzee wenu amewatumikia Watanzania kupitia Chadema kwa miaka 21 mfululizo bila malipo. Leo hapa tujiulize wangapi tunaweza kufanya hivyo,” alisema.
Mzee Bob Makani alizikwa jana katika Kijiji cha Ukenyenge, Tarafa ya Negezi, wilayani Kishapu, eneo la makaburi alipozikwa Baba yake, marehemu Ali Makani na ndugu zake wengine.
Source:Jamii Forums.
Post a Comment
CodeNirvana